Na Danson Kaijage
DODOMA:SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikiwa kudhibiti upotevu wa umeme kutoka asilimia 15.3 kwa mwaka 2021 hadi asilimia 14.54 kwa mwaka 2025.
Udhibiti huo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Gissima Nyamo – Hanga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Amesema Shirika hilo lilikuwa likikumbana na upotevu wa umeme kwa kiwango hicho lakini kutokana na juhudi za serikali iliyopo madarakani imefanikisha kupunguza upotevu wa umeme njiani.

Mkurugenzi huyo amesema hatua ya kupunguza upotevu wa umeme inaongeza tija ya matumizi ya nishati hiyo kuwa ya uhakika na kurahisisha shughuli za watumiaji wa nishati hiyo muhimu.
Mafanikio mengine ya TANESCO ni kuongezeka kwa vituo vya kupokea na kupoozea umeme kutoka vituo 128 kwa mwaka 2021 hadi kufikia vituo 139 kwa mwaka 2025.
Amesema l hatua hiyo ni kubwa ambayo inatoa urahisi wa kutoa umeme mkubwa sehemu moja na kuupeleka katika vituo vya kupozea umeme na kuwa tayari kwa mlaji au mtumiaji.

Vile vile amesema sababu za kukatika kwa umeme katika treni ya mwendakosi (SGR) inatokana na ugeni wa kuwepo kwa usafiri huo nchini.
Amesema ili kumaliza changamoto hiyo Shitika lipo mbioni kuanzisha Mkoa maalumu kwa ajili ya kushughulikia changamoto za umeme katika treni hiyo.
Amesema hatua hiyo itatatua changamoto hiyo, pia atakuwepo Meneja Uratibu ambaye atakuwa akishughukia mradi huo pekee pamoja na timu maalumu.
Amesema kwa kipindi cha mwaka 2021 wateja walikuwa milioni 3.1 na kufikia mwaka 2025 wateja ni milioni 5.39 sawa na ongezeko la wateja wapya milioni 2.2 ndani ya miaka minne.