Na Lucy Ngowi
SINGIDA: HALMASHAURI ya Wilaya ya Singida imepokea Madaktari Bingwa watatu na Wauguzi Wabobezi wawili kwa ajili ya kuwajengea uwezo zaidi madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Wilaya kwenye eneo la kina mama na watoto.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ya Singida Dkt. Dorisila John amesema hayo baada ya madaktari hao na wauguzi kuhitimisha mafunzo yao katika Hospitali hiyo ya Wilaya ya Singida.
Kwa ujio wa madaktari bingwa hao na wauguzi wa Mpango wa Mama Samia, Dkt.Dorisila ameishukuru serikali kwa kazi kubwa inayoifanya katika sekta ya afya nchini.
“Ugeni huu umefika Machi 17 mwaka huu 2025, umekuwepo kwa siku tatu hadi Machi 19. Tumeshukuru kwa sababu wataalamu hawa wametoa elimu nzuri, ujuzi na maarifa na watumishi wetu wamefurahi,” amesema.
Ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na maono hayo kwa kupeleka Madaktari Bingwa na Wauguzi Wabobevu katika maeneo yenye uhitaji wa utaalam zaidi.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi kutoka Mkoani Mwanza Wilaya ya Nyamagana amesema wamekuwepo Singida kwa ajili ya kutoa mafunzo ili kupunguza vifo vya kina mama na watoto katika wilaya zote mkoani Singida.
“Tupo 20 tumegawanyika wengine wamekwenda katika wilaya nyingine, na sisi tupo watano hapa katika Hospitali ya Wilaya ya Singida,” amesema.
Amesema miongoni mwao wapo madaktari bingwa watatu waliobobea kwenye magonjwa ya kina mama, magonjwa ya watoto na wa usingizi na ganzi salama.
Pia timu yao ina wauguzi wawili mmoja akiwa muuguzi mkunga na mwingine wa chumba cha upasuaji.
” Lengo la kuwepo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo watoe huduma bora, hususan eneo la mama na mtoto, ili kupunguza vifo vya mama, wajawazito na watoto wachanga,” amesema.
Amesema timu yao imewafikia watumishi 46 na kila mmoja amepata mafunzo tofauti.
Amesema ni imani kwamba waliyofundishwa wayayafanyia kazi.
Wanamshukuru Rais Samia kwa jitihada anazofanya katika sekta ya afya, kwajinsi alivyoona anaweza kupunguza vifo hivyo.
Watumishi wa afya walioshiriki wameeleza shukrani zao kwa madaktari hao kwa ujuzi waliopata na wameahidi kutumia maarifa hayo kuboresha utoaji huduma na kuongeza weledi katika kazi zao za kila siku.
Mpango huu ni moja ya juhudi za serikali za kuimarisha huduma za afya nchini na kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma bora na salama.