Na Mwandishi Wetu
DODOMA: MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kujivunia kasi ya ufanisi na mafanikio ya kiutendaji katika kuongeza wanachama, kukusanya michango, kuwekeza, kulipa mafao pamoja na kuboresha huduma kwa wanachama katika miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumzia mafanikio ya NSSF yaliyopatikana katika miaka minne ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema wanajivunia kuongeza thamani ya Mfuko kutoka Sh. Trilioni 4.8 Februari 2021 hadi kufikia Sh. Trilioni 9.2 Februari 2025.

Mshomba amesema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, mapato yatokanayo na michango na kukua kwa thamani ya vitega uchumi vya Mfuko, ambayo yanachagizwa na juhudi za Serikali katika kufungua nchi na kuruhusu wawekezaji nchini.
Amesema Mfuko umeandikisha wanachama wapya 1,052,176 ikiwa ni ongezeko la asilimia 50, ambapo idadi ya wanachama wachangiaji imeongezeka kwa asilimia 106 kutoka 849,886 waliokuwepo mwaka 2021 hadi 1,758,018 Februari 2025.
Mshomba amesema katika kipindi hicho, michango iliyokusanywa imeongezeka kutoka Sh. Trillioni 1.13 Februari 2021 hadi kufikia Sh. Trillioni 2.15 Februari 2025 sawa na ongezeko la asilimia 90.

Vilevile, thamani ya vitega uchumi vya NSSF imeongezeka kwa asilimia 92 kutoka trilioni 4.28 mwezi Februari 2021 hadi kufikia trilioni 8.21 Februari 2025.
Amesema katika kipindi husika, Mfuko umelipa mafao ya Sh. Trilioni 3.10 na kuwa malipo ya mafao kwa mwaka yaliongezeka kwa asilimia 69 kutoka Sh. Bilioni 537.08 Februari 2021 hadi kufikia zaidi ya Sh.Bilioni 909 Februari 2025.
Ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na Mfuko kufanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali imeongeza ufanisi wa malipo ya mafao kutoka asilimia 78.2 Februari 2021 hadi asilimia 96 Februari 2025,” amesema.
Pia amesema NSSF kupitia kampuni tanzu ya Mkulazi, imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi mwezi Novemba 2023 ambacho hadi kufikia mwezi Februari 2025, jumla ya tani 19,124 za sukari zimezalishwa. Mradi huo umeajiri watu 8,302 na unachangia megawati 15 za umeme kwenye gridi ya Taifa.
Ameishukuru Serikali kwa kuwaondolea kero wananchi wa Kigamboni ambao tozo za kupita katika Daraja hilo zimepunguzwa ambapo bodaboda wanalipa shilingi 300 badala ya 1,500 na daladala shilingi 1,500 badala ya 3,000.
Kuhusu miradi ya nyumba na hoteli, Mshomba amesema wanaendelea na utekelezaji wa miradi ya nyumba ya Dungu, Toangoma, Kijichi III pamoja na hoteli ya Mzizima na Mwanza ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2025 na Juni 2026.
Akizungumzia Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri, amesema kupitia mpango huo wananchi wanaweza kujiunga na kuchangia kwa hiari katika Mfuko na kunufaika na mafao pamoja na huduma nyingine zinazotolewa.
“Nawaomba wananchi wenzangu wachangamkie fursa ya kujiunga na NSSF kupitia skimu hii ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Aprili, 2025 ambapo kwa sasa tunaendelea na Kampeni tuliyoipa jina la “NSSF Staa wa Mchezo” unaweza kujiunga na kuchangia kwa kubofya *152*00# kima cha chini ni Sh.30,000 na kuendelea,” amesema.
Amesema mfuko unatambua mchango na ushirikiano unaopata kutoka kwa waajiri na wanachama na kuwa ni sehemu ya mafanikio hayo yaliyopatikana katika Serikali ya awamu ya sita.