Na Danson Kaijage
DODOMA: HOSPITALI ya Benjamini Mkapa (BMH), imepandikiza mimba kwa wanawake 21 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha BMH imeweka vipandikizi maalum kwenye uume kwa wanaume watano.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa Profesa, Abel Makubi amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema wanawake hao waliopandikizwa mimba ni kati ya miaka 35 hadi 50.
Amesema wahitaji hao ni wale waliokuwa wakihangaika juu ya kupata mimba lakini hawakufanikiwa, lakini wamekuwa na uhitaji wa kupata watoto na wamekosa kwa njia ya kawaida.
Kwa upande wa wanaume ambao wamewezeshwa kupatiwa vipandikizi maalumu kwa kuhimarisha uume ni watano na hao ni wachache kutokana na tatizo la nguvu ya kiume kuwa kubwa lakini pia gharama ya matibabu kuwa kubwa zaidi.
Amesema gharama ya kuwekewa vipandikizi maalumu kwa ajili ya kuhimarisha nguvu za kiume ni kati ya Sh Milioni tano hadi sita.
Akielezea mafanikio mengine ya hospitali hiyo ni pamoja na uboreshaji na juongeza huduma za tiba za Kibingwa na Ubingwa wa Juu.
Hivyo kuokoa kiasi cha Sh. Bilioni 2.8 ambazo zingetumika kuwapatia rufaa wagonjwa ambao wangeenda hospitali za nje kupatiwa matibabu ya figo.
Amesema kuwa kwa sasa hospitali ya Benjamini Mkapa imekuwa ikitoa huduma ya upandikizaji figo pamoja kuvuna figo ambapo huduma hiyo ilikuwa ikipatiana nje ya nchi na sasa inapatikana nchini.
Ametaja huduma zinazotolewa hospitalini hapo mpaka sasa kuwa ni
upandikizaji figo, upandikizaji uloto, upasuaji wa mishipa ya damu, upasuaji wa Moyo kwa kufungua kifua na uvunjaji wa mawe kwenye mfumo wa mkojo kwa kutumia mawimbi.
Huduma nyingine alizotaja kuwa ni upandikizaji uume, upasuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu, upasuaji wa uti wa mgongo, kubadilisha nyonga na magoti, upasuaji wa matundu madogo, matibabu ya mfumo wa chakula na matibabu ya magonjwa ya figo.
Huduma nyingine ametaja kuwa ni uchujaji damu , matibabu ya magonjwa ya Moyo, uchunguzi na matibabu ya mishipa ya moyo kupitia maabara ya uchunguzi, uchunguzi na matibabu ya kiradiolojia, Tiba ya magonjwa ya Hormone na kisukari na huduma za upandikizaji Mimba .
Pia amesema kuwa Hospitali ya Benjamini Mkapa imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 25 kati ya 50 kwa ndani ya miaka minne kwa gharama ya Sh Milioni 875, kati ya hao wagonjwa 10 wamelipiwa matibabu haya kupitia mfuko maalum wa Samia Suluhu Hassan kwa kiasi cha Sh. Milioni 350.