Na Mwandishi Wetu
SINGIDA: MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elim una Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore amesema kuwa mamlaka hiyo inaadhimisha miaka 30 tangu ilipoanzishwa mwaka 1995.
Kasore amesema hayo katika Chuo cha VETA, mkoani Singida kwa maelezo kuwa maadhimisho hayo yataangazia mafanikio, changamoto na mustakabali wa elimu ya elimu ya ufundi stadi nchini.

Amesema katika kipindi cha maadhimisho vyuo vya VETA vilivyopo kwenye mikoa na wilaya nchini kote vitatoa huduma ya ufundi ya ukarabati wa miundombinu ya Serikali bure ikiwemo majengo ya hospitali, zahanati, shule, ofisi za umma pamoja na kwa watu wasiojiweza, ili kuonyesha mchango wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwenye jami.
“Wanafunzi, walimu na wahitimu watatoa huduma za kiufundi kama kupaka rangi majengo yaliyochakaa, kurekebisha mifumo ya umeme, mifumo ya mabomba ya maji, milango na samani,”amesema.
Amesema maadhimisho hayo yataimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ya elimu ya ufundi.
Amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika kwa siku nne, kuanzia Machi 18 hadi 21, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ambapo kutakuwa na maonesho ya kazi na ubunifu wa wanafunzi, mashindano ya ujuzi, kongamano la wadau, na utoaji wa tuzo kwa taasisi na watu binafsi waliochangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya ufundi stadi nchini.
“Miaka 30 ya VETA ni ushuhuda wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata ujuzi bora wa ufundi stadi unaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa. Katika miaka hii, tumeweza kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa,” amesema.
Amesema, kwa miaka 30, VETA imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kujenga vyuo vipya, kupanua fursa za mafunzo kwa makundi maalum, na kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Amesema idadi ya vyuo vinavyomilikiwa na VETA imeongezeka kutoka 14 mwaka 1995 hadi 80 mwaka 2025, huku vyuo vingine 65 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Pia sekta za mafunzo zimeongezeka kutoka 10 mwaka 1995 hadi 13 mwaka 2025, zikihusisha fani 89 zinazohitajika katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa kisasa.