Na Danson Kaijage
DODOMA: KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Emmanuel Nchimbi, ameonya tabia ya baadhi ya wanachama walioanzisha utamaduni wa kutengeneza makundi,
Makundi ambayo yanatoa matamko ya kuwataka baadhi ya wanasiasa ndani ya chama hicho kuwa wagombea pekee jambo ambalo halikubaliki.

Nchimbi amesema hayo leo Februari 19, 2025 alipofungua mafunzo kwa makatibu tawi,kata,wilaya na Mkoa katika Mkoa wa Dodoma.
“Wapo wanachama watakao gombea na watakao hamasisha matamko kwenye maeneo yao ili wawe wagombea pekee wagombea hao watahamasisha kuenguliwa kwa majina yao kirahisi.
“Pia wapo wagombea ambao wameanzisha utaratibu wa kutengeneza makundi ya kutoa matamko mbalimbali ya kulazimisha asijitokeze mgombea mwingine kuwania nafasi fulani ya uchaguzi.
“Na wengine wanatengeneza sherehe za kumbukizi ya kuzaliwa kwa bini yake na kuwaalika wana CCM na kuwalipa posho huku wakiwa wamevalia nguo za kijani,watu wa aina hiyo watakatwa majina yao mapema na wala wasidhani kuwa wataonewa huruma,” amesema.
Akizungumzia hilo amesema, kuna mchezo wa mtu kuandaa sherehe ya kufanya kumbukizi ya ndoa kwa kutimiza miaka mitano wakati ndoa ina miaka mitatu na anakuwa na ujasiri wa kualika wana CCM 300 na kuwalipa posho jambo abalo linaonesha wazi kuwa hatua hiyo ni ushawishi wa rushwa.
Amesema uongozi wa CCM umeanza kufuatilia matukio ya aina hiyo na iwapo uongozi utajiridhisha kuwa kuna mgombea anafanya vitendo vya kutoa rushwa au kusingizia kufanya sherehe na matamko mgombea huyo hataweza kupenya.
Amewataka makatibu ambao watakuwa sehemu ya usimamizi wa uchaguzi kufuatilia matukio, kuweka rekodi vizuri ili pale itakapo bainika kutokea mambo hayo atakayekuwa anagombea achujwe mapema.

Pia. amesema,”Kuna watu wanatenga laki tano tano na kuwahesabu wajumbe 300 kwa kuwahonga na wanapopata uongozi wanakuwa hawafanyi kitu chochote kwa madai kuwa wao walimaliza mchezo kwa kuwanunua .
“Wote mnajua kuwa uchaguzi unaweza kuwa mgumu kulingana na watu mliowachagua na tabia zao,mlevi anaweza kupita barabarani anayumba lakini hakuna wa kumsema lakini ukiwa umevaa sare yako ya chama na ukaonekana umelewa utapigwa picha na kuwekwa mitandaoni na kuanza kueleza kuwa kigogo wa CCM akutwa amelewa chakali”amesema.
Nchimbi amesema CCM kinataka kupata viongozi makini na wachapa kazi ambao watakuwa kinyume na masuala ya rushwa sambamba na kutokuchafuana kati ya waliopo madarakani na wale wanaotaka kuingia.