Na Mwandishi Wetu
DODOMA: KANISA la Mlima wa Nuru Calvary Assembeles of God (CAG) lililopo Chamelo Nzuguni B Jijini Dodoma limeanzisha maombi ya kimkakati kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa amani na upatikanaji wa viongozi sahihi ifikspo Oktoba 2025.
Katibu wa Kanisa hilo, Dkt. Mussa Aliingonoti amesema hayo, wakati wa matangazo kwa waumini na kueleza kuwa ni wajibu wa kanisa kuliombea taifa hususani kwa kipindi ambacho kinaelekea katika uchaguzi mkuu.

Amesema kanisa hilo limekuwa na maombi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na maombi ya kuliombea kanisa la mahali pamoja na watumishi kwa ujumla sambamba na kuombea ujenzi wa kanisa linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Dk.Alingiinoti amesema kanisa linalo wajibu mkubwa wa kuhakikisha linaomba kwa maana ya kuhusimika ufalme wa Mungu duniani kwa kuyaombea makundi mbalimbali pamoja na kuliombea taifa kwa ujumla wake ili kwa na viongozi sahihi ambao ni wacha Mungu.
“Kanisa la Mlima wa Nuru limeamua kuanzisha maombi ya kimkakati kwa nia ya kuliombea kanisa na kuombea ujenzi wa kanisa jipya pamoja na kuliombea taifa na uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu kwa nia ya kuwapata madiwani,wabunge na Rais pamoja na viongozi mbalimbali wa ngazi ya kuchaguliwa.
“Kwa sasa tunaelekea katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi wa kada mbalimbali na ili kupata viongozi walio wema na wenye sifa na wenye hofu ya Mungu ni lazima kufanya maombi kwa ajili ya kupata viongozi waliowacha Munu,” amesema.
Amehimiza waumini kufanya maombi kwa dhati ili kuliombea kanisa, jamii na taifa, kupata viongozi wenye hofu ya Mungu na wale ambao hawatakuwa kwazo kwa taifa.