Na Mwandishi Wetu
SAUDI ARABIA: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ameshukuru ushirikiano uliopo baina ya wadau wa maendeleo ya kazi bila kusahau miongozo na mabadiliko ambayo yamefanyika nchini Tanzania.

Aidha mabadiliko yaliyofanyika ni pamoja na mikakati ya kukuza ujuzi, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA), mkazo katika miradi inayotoa ajira nyingi na ile ya kimkakati.
Ridhiwani ametoa shukrani hizo wakati akichangia kwenye kikao maalum cha Mawaziri mbalimbali duniani katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Soko la ajira Januari 29, mwaka huu 2025 Jijini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Ridhiwani amesema mkutano huo unawakutanisha Mawaziri wa Kazi na Ajira kutoka nchi zaidi ya 45 duniani kujadili na kuweka mikakati ya kuongeza kazi za staha kwa Vijana kwa kuzingatia mchango wa sayansi na teknolojia.