Na Lucy Ngowi
PWANI: WAAJIRI wengi katika Sekta Binafsi wamekuwa wakiwazuia wafanyakazi wao kujiunga na Vyama vya Wafanyakazi, kwa kuhisi wakijiunga watakuwa tishio.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania ( TUGHE), Hery Mkunda amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Habari wa Mfanyakazi Tanzania.
Mkunda ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA), amesema kutokana na hali hiyo wamechukua hatua kwa kushirikiana na serikali kupitia Ofisi ya Kamishna wa Kazi kuhakikisha wanaendelea kufanya kaguzi sehemu mbalimbali za kazi.
“Pia tunazungumza na waajiri waruhusu wafanyakazi wao kujiunga na vyama maana ni haki yao kwa mujibu wa mikataba ya Kimataifa ambayo Sisi Tanzania tumeisaini,” amesema.
Mkunda pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika Mashariki, pia Mjumbe Kamati Kuu ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Duniani.