Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: SERIKALI ya Tanzania imeihakikishia Uingereza, kuendeleza ushirikiano kwenye sekta ya madini hususani katika kujengea uwezo watu wake, kubadilishana uzoefu, uongezaji thamani madini na kuwekeza kwenye kufanya tafiti mbalimbali ili kukuza sekta hiyo.
Vile vile kupanua mnyororo wa thamani ili kuongeza ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la taifa.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema hayo Mkoani Dar es Salaam, alipofanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young.

Amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kuwajengea uwezo watu wake na kubadilishana uzoefu hususani katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini nchini (GST) na British Geological Survey (BGS) ya Uingereza.
Eneo lingine la ushirikiano amesema ni lile la uongezaji thamani madini mkakati ambapo Tanzania imejipanga kuhakikisha inavutia uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani.

“Tupo katika hatua za mwisho kukamilisha mkakati huu maalum wa madini mkakati na muhimu ambao pia ni sehemu ya Kampeni ya Dunia katika kupunguza hewa ya ukaa kupitia matumizi ya nishati safi,” amesema.
Akizungumza katika Mkutano huo Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Young amesema Uingereza inapongeza jitihada kubwa za kukuza sekta ya madini zinazofanywa na serikali ya Tanzania.
Balozi huo ameahidi kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo hasa katika kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo.

Amesema Uingereza itashirikiana na Tanzania kwa ukaribu ili malengo hayo yatimie.