JANUARI 29,2024: Lema: nitagomba ubunge 2025 nipate thawabu kwa Mungu
MBUNGE wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amesema mpango wake wa kugombea ubunge katika uchaguzi ujao si kwa ajili ya kazi hiyo kumpatia kipato bali kufanya kazi hiyo ili apate thawabu kwa Mungu kwa kupigania haki za watu.
Alisema hayo wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha medani za siasa kinachorushwa na Star Tv.
JANUARI 29,2024:Wananchi wahoji ahadi za Askofu gwajima Kawe
Baadhi ya wananchi wa Kawe wamehoji kuhusu utekelezaji wa ahadi alizotoa mbunge wao, Askofu Josephat Gwajima wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2020.
FEBRUARI 7, 2024: Lissu azuiwa redion, Nape atoa neno
Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye amesema Serikali ya awamu ya sita haijawahi na haina mpango wa kuminya uhuru wa Vyombo vya Habari ambapo amevitaka Vyombo hivyo kuwapa nafasi Wanasiasa wote bila kujali tofauti ya Vyama vyao.
Akizungumza Jijini Dodoma leo, Nape amesema “Serikali imeona kuhusu Wasafi FM kuzuia mahojiano kati ya Tundu Lissu na Radio hiyo na maelezo yaliyotolewa yalisema wamezuia kwa maelekezo kutoka juu lakini baadaye nimeona Lissu mwenyewe akisema amepewa taarifa kwamba ilikuwa ni mkanganyiko wa ndani wa Wasafi”
“Serikali inatoa taarifa kwamba toka Rais Dkt. Samia Suluhu ameingia madarakani ameimarisha uhuru wa Vyombo vya Habari na Demokrasia, kilichotokea leo kimetusikitisha hasa kauli kuwa ni maelekezo kutoka juu, Serikali ya Rais Samia haijafanya na haina mpango, tuondokane na hofu ya kujifungia sehemu na kuwa na visingizio kwamba kuna maagizo, kuna Serikali inafanya hivi hapana”
FEBRUARI 8,2024: Samia mabalozi msiingilie uchaguzi
Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya mabalozi kuacha kuingilia uchaguzi na badala yake waheshimu miiko ya diplomasia.
Rais Samia ameyasema hayo katika sherehe za mwaka mpya 2024 kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa zilizofanyika Ikulu.
“Serikali itaendeza ushirikiano na balozi zote kwa mujibu wa katiba, tunu za kitaifa, usawa, umoja na mshikamano wa kitaifa….; “Msiingilie uchaguzi wetu, kuzingatia mila, kanuni na maadili ya diplomasia.” amesema.
MACHI 13, 2024:Uchaguzi kanda chadema moto
UCHAGUZI wa kanda za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ‘ni wa moto’, safari hii kuna usaili maalum kwa wagombea katika kanda nne zinazotarajiwa kufanya uchaguzi hivi karibuni.
Jana wagombea wote katika nafasi hizo pamoja na wanaogombea kwenye mabaraza yake kutoka kwenye kanda hizo waliitwa makao makuu ya chama hicho kwa ajili ya usaili na Kamati Kuu ya chama iliyoanza vikao vyake Mei 11, mwaka huu.
APRIL 22,2024: Makonda aitwa Kamati ya maadili CCM
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, leo anatarajia kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma.
JULAI 29,2024: Kinana ajiuzuru uongozi CCM, Samia aridhia
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amejiuzulu wadhifa huo baada ya kuomba mara kadhaa kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan ambaye sasa ameridhia ombi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Julai 29, 2024 na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala imesema Kinana ameandika barua ya kuomba kupumzika.
Katika majibu yake Mwenyekiti wa CCM Samia amesema: “Ni kweli nilipokuomba utusaidie kwa nafasi ya makamu mwenyekiti nilikuahidi utakaa muda mfupi kama ulivyoomba, na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia lakini kwa kuwa umeomba sana na ahadi ni deni nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujiuzulu kwako.”
OKTOBA 7,2024: Siri Boni Yai kushinda akiwa mahabusu
ALIYEKUWA Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob maarufu kwa jina la Boni Yai, ameshinda nafasi ya Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kupata kura 60, sawa na asilimia 77, akiwa mahabusu gerezani.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Kanda ya Pwani, Kerenge Jerry alisema mshindani wake wa karibu, Gervas Lyenda alipata kura 17 sawa na asilimia 23. Wengine waliochaguliwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee CHADEMA (BAZECHA), James Haule, Makamu Mwenyekiti, Wilson Katunzi, huku Katibu akichaguliwa Deogratius Kajula.
Oktoba 10, 2024 Uandikishaji uchaguzi wa mitaa kuanza leo
Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wote wenye sifa kujiandikisha kwenye Orodha ya Wapiga kura wa Serikali za Mitaa kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024.
Samia ameyasema hayo wakati alihutubia wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa mkoani Ruvuma katika mkutano uliofanyika viwanja vya Bandari ya Mbambabay.
Amesema ili uwe mpigakura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ni lazima uwe umejiandikisha kwenye Orodha ya Wapigakura wa Serikali za Mitaa ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia tarehe 11-20/10/2024 nchi nzima na uandikishaji utafanyika kwenye vijiji/vitongoji pamoja na mitaa.
OKTOBA 15,2024: Samia: Tusichukulie poa uchaguzi mitaa
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kutokuchukulia poa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu na kuwa ndio utaleta taswira nzima ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na kueleza ni fursa kubwa ya kukuza demokrasia na ushiriki katika maendeleo ya jamii.
NOVEMBA 13, 2024: Samia aingilia kati wagombea kukatwa
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, ameingilia kati malalamiko ya vyama vya upinzani kudai wagombea wao wameenguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupuuza kasoro ndogo ndogo zilizofanywa na wagombea wa vyama vya siasa wakati wa kujaza fomu kwa ajili ya uchaguzi huo unaohusu serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwapo wa wagombea wengi wa vyama vya siasa kuenguliwa kutokana na makosa madogo waliyoyafanya wakati wa kujaza fomu.
DISEMBA 12,2024: TUNDU LISSU ACHUKUA FOMU UENYEKITI CHADEMA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).Tundu Lissu ametangaza nia ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.c
Akizungumza na wanahabari leo katika ukumbi wa Mlimani City mjini Dar es Salaam, Tundu Antipas Lissu, amesema anaitaka nafasi hiyo ambayo inashikiliwa na Freeman Mbowe tangu mwaka 2004.
“Ninapenda kuamini kwamba, ninyi wanachama wenzangu mnaamini nina sifa za kutosha za kugombea nafasi ya juu ya uongozi katika chama chetu,” amesema Tundu Lissu ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti wa chama hicho.
Imeandaliwa na Lucy Ngowi