Na Lucy Ngowi
DODOMA: MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini kuwahimiza waajiri kuwasilisha taarifa mapema pindi wafanyakazi wao wanapopata ajali au ugonjwa wakiwa kazini, kuharakisha upatikanaji wa fidia stahiki na kwa wakati ikiwemo fao la matibabu.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Mkurugenzi wa Uendeshaji wa mfuko huo Anselimu Peter amesema fidia zinazotolewa na mfuko huo ni mtiririko wa mafao mbalimbali ikiwemo matibabu ambayo hayana ukomo.
Pia amesema vyama vya wafanyakazi vina haki ya kutoa taarifa WCF kuhusu ajali au ugonjwa unaotokana na kazi endapo mwajiri atashindwa kufanya hivyo.
“Fidia ni mtiririko wa mafao, ambapo fao la kwanza ni la matibabu, sasa mtu akipata ajali au ugonjwa unatokana na kazi tunawaomba nyie muwe chachu ya kuwahimiza waajiri kutoa taarifa mapema katika WCF ili aweze kupata stahiki zake ikiwemo za matibabu.
“Matibabu haya yanaanzia katika hospitali zote ikiwemo Kanda, Taifa na hata Nje ya Nchi,” amesema.
Vile vile amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuwahimiza wafanyakazi wanaopata madhila wakiwa kazini kuwasilisha nyaraka kwa wakati ili Mfuko uweze kufanya tathmini mapema na wahusika walipwe fidia kwa wakati.
Amesema mfuko umechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa huduma zake zinapatikana kwa njia ya mtandao ili kurahisisha ikiwemo uwasilishaji wa taarifa na nyaraka muhimu.
“Tumeweka mifumo mbalimbali ya kielektroniki ili kurahisisha utoaji wa huduma zetu. Zaidi ya asilimia 90 ya huduma zetu zinapatikana kwa njia ya kielektroniki, ambapo mteja wetu anaweza kupata huduma zetu popote pale alipo,” aliongeza Mha. Peter.