Na Lucy Lyatuu
WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kuchangamkia soko la Huru la Afrika (AfCFTA) kwa kupeleka bidhaa aina ya batiki kwa kuwa inakubalika na inaongeza ushindani.
Rais wa chemba ya wanawake wafanyabiashara nchini (TWCC), Mercy Silla amesema hayo Dar es Salaam katika mafunzo kwa wajasiriamali, yaliyoandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa kudhaminiwa na GIZ.
Amesema kuna mazao kama kahawa,korosho yyanakubalika lakini ni muhimu kutambua kuwa ni vyema wanawake kupeleka batiki kontena kwa kontena kwani fursa ipo.
Amesema batiki za Tanzania zinakubalika hivyo wafikirie yaliyo chanya, na kujituma kwani kufanya hivyo watapiga hatua.
Aidha amesema tayari zipo Kamati mbalimbali zinazoshuhulikia vikwazo visivyo vya Kiushuru kwa kila nchi ili kuwezesha wajasiriamali kupeleka bidhaa zao katika eneo huru la biashara.
Amesema vipo vikwazo vilivyoondolewa kwani kila nchi ilikuwa na taratibu zake, kwamba wana masuala yao ya kodi, ushuru, n ahata viwango vyao vya ada ambavyo hivyo vinaendelea kurekebishwa ili kuwe na mifumo inayofanana.
“Lakini kuna makubaliano kuwa vikwazo hivyo visizue kuwe na taratibu zinazofanana ili soko hilo liwe huru kufanya biashara na rahisi kuingia na kufanya biashara,” amesema.
Amesema ziko kamati mbalimbali zinafanyia kazi hatua kwa hatua lakini vikwazo vingi safari hii vimeshaanza kufanyiwa kazi ndio maana watu wameingia kwenye soko.
Amesema mafunzo kwa wajasiriamali yanalenga kuwapa taarifa muhumu za kuingia kwenye soko hilo la afrika ambapo nchi ya Tanzania imeridhia.
“Soko ni kubwa, wakuzwe, waungane ili wazalishe bidhaa kwa wingi na tunawafundisha namna ya kurasimishe biashara ili wajasiriamali wajiunge kwa Pamoja na kuingia kwenye soko,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika laViwango Tanzania (TBS) Lazaro Msasalaga amewataka wajasiriamali kuzingatia viwango udhibiti na ubora kwenye bidhaa zao kwa kuwa ni eneo muhimu linalosaidia kulinda soko la bidhaa na kuongeza ushindani kwenye masoko ya kikanda na kimataifa ikiwemo soko huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Amesema Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kujenga misingi shindani na endelevu kwa viwanda na watoa huduma wenye kuwezesha biashara ndogondogo kwa kuzingatia rasilimali zilizopo nchini.
“Miundo mbinu ya huduma Pamoja na kuzingatioa viwango ni eneo muhimu la kuchangia ukuaji wa maendeleo ya viwanda uwekezaji na biashara,” amesema.
Mwakilishi kutoka Sekretarieti ya EABC, Moses Kanyesigye amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wajasiriamali ili kuwafunisha kuhusu soko suala zima la ubora na viwango.
“Tunataka wajasiriamali kupata nafasi kwa soko hilo na bidhaa zao kufika huko, Tunawafunidisha namna ya kutengeneza bidhaa zao ziweze kufika katika soko hilo,” amesema.
.