Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imenufaisha wadau wa kilimo kutokana na kugundua mbegu bora zilizofanyiwa utafiti katika mazao mbalimbali yakiwemo ya karanga,maharage na mtama.
Wadau hao ni wakulima, wazalishaji mbegu na wasindikaji wa bidhaa za kilimo wamekiri kunufaika na utafiti huo wa mbegu bora na za kisasa uliowaongezea tija katika mnyororo wa thamani wa mazao hayo.
Katika mkutano uliofanyika Dodoma wa kutoa matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika zinazobaini uhitaji wa soko na kusambaza mbegu mpya za mtama, maharage na Karanga, wadau hao wa kilimo wameeleza hayo.

Mzalishaji wa mbegu za karanga na mtama kutoka Chamwino Dodoma, Olipa Mahala amesema alipokuwa akilima mbegu za kienyeji alikuwa anavuna gunia nne mpaka tano kwa hekta lakini alipoanza kulima mbegu ya mtama ya TARISOR 1 anavuna wastani wa gunia 15-20 kwa hekta.
Naye Msindikaji wa siagi ya karanga kutoka Bahi mkoani hapa, Kadala Komba amesema utumiaji wa mbegu za Naliendele 2016 umuongezea tija kwa kupendwa sokoni kutokana na ladha pamoja na rangi yake.
Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI- Dkt. Thomas Bwana amesema taasisi hiyo imegundua mbegu mbalimbali, imeendelea kufanya tafiti zaidi ili kugundua teknolojia zinazojibu changamoto za wakulima na wadau katika mnyororo mzima wa thamani.
Mkurugenzi wa Idara ya Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano wa TARI, Dkt. Sophia Kashenge amesema taasisi hiyo haishii kugundua bali pia kuhakikisha mbegu hizo zinawafikia wakulima kupitia njia mbalimbali.

Njia hizo ni uanzishaji wa mashamba darasa, kutoa elimu kwa maofisa ugani, wakulima, wazalishaji mbegu na wafanyabiashara wa mbegu na wasindikaji wa bidhaa.
Miongoni mwa mbegu ziligunduliwa na TARI ni aina mpya za mbegu za Maharage; TARIBEAN 6, TARIBEAN 7, TARIBEAN 8, TARIBEAN 9, TARIBEAN 10 na TARIBEAN 11.
Karanga aina za; TARIKA 1 na TARIKA 2 pamoja na mtama TARISOR 1 na TARISOR 2.