Na Lucy Ngowi
MKURUGENZI waTume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Usekelege Mpulla amesema kati ya migogoro inayopokelewa miongoni mwao ipo ya wafanyakazi wa majumbani, huisikiliza na kuitendea haki.
Amesema hayo alipozungumza na MFANYAKAZI kuhusu tume hiyo endapo kama imekuwa ikipokea migogoro ya wafanyakazi hao kwa ajili ya kusikiliza ili sheria iweze kuchukua hatua.
Mpulla amesema, “Tunapozungumzia Hakikazi Tanzania hakuna mfanyakazi aliyebaguliwa. Haijalishi mfanyakazi ni wa kada gani kwani sheria imempa haki zote,”.
Pia amesema anapozungumziwa mfanyakazi wa ndani sheria iliyopo haijamtenga, “Tunapozungumzia haki, maslahi, mgogoro wa kikazi bado ana haki,”.
“CMA haijawatenga wafanyakazi wa ndani, tunatoa wito wafahamu haki zao zimelindwa kisheria. CMA inafungua milango kwa wafanyakazi hao endapo wakiachishwa kazi, wakilipwa kima cha chini, pia wasipolipwa,” amesema.
Ameongeza kuwa hivi karibuni wamekuwa wakizungumzia mfumo wa utatuzi wa migogoro na usajili wa migogoro, hivyo mfanyakazi aliyeona vigumu kufikia tume, atajisajili mgogoro wake kupitia mfumo huo.
Amesema mfumo huo ukitumika mfanyakazi atakayekuwa ameona vigumu kufika kwenye tume hiyo ataweza kujisajili kupitia mfumo.
Amesema katika Sheria za Kimataifa zinazosimamiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO), kuna mkataba namba 189 umebainisha hizo haki kwamba wafanyakazi wa majumbani wapewe mikataba.
“Hivi sasa tunafanyakazi kwa karibu na ILO. Kuna Mradi unakuja kutakuwa na mpango mkubwa wa kuwafikia wafanyakazi wa ndani na haki zao zinafikiwa,” amesema.
Pia amewataka wafanyakazi hao kutokusita kufika CMA endapo wanaona hawajatendewa haki na waajiri wao.