Na Mwandishi Wetu
TANGA: WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amesema tangu kufanyika kwa maboresho ya Sheria na Kanuni za Madini kupitia Tume ya Madini, Wizara hiyo imeongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli kutoka mwaka hadi mwaka.
Mavunde ameyasema hayo katika kikao alichofanya na Menejimenti ya Tume ya Madini, Wakurugenzi, Mameneja na Maofisa Madini wakazi wa mikoa, chenye lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha Sekta ya Madini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.
Uimarishaji huo ni kupitia ukusanyaji wa maduhuli, udhibiti wa utoroshaji wa madini, udhibiti wa mianya ya upotevu wa makusanyo na kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Amesema siri ya kasi hiyo inatokana na
ubunifu wa ukusanyaji wa maduhuli kwa kudhibiti mianya ya utoroshaji wa madini.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri sana ya ukusanyaji wa maduhuli hasa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi sasa ambapo kiasi cha Sh. Bilioni 196 zimekusanywa, kiasi ambacho kinazidi kiasi kilichokusanywa kwa mwaka mzima wa fedha wa mwaka 2015/2016,” amesema.

Kutokana na mafanikio hayo, amesema kiasi hicho cha pesa kilichokusanywa cha sh. Bilioni 196 kwa kipindi cha miezi miwili kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ni zaidi ya kiasi cha Sh. Blioni 161 kilichokusanywa kwa mwaka mzima wa fedha 2015/2016.
Kwa upande mwingine Mavunde ameipongeza serikali kwa kutoa kipaumbele katika sekta hiyo kwa kuongeza bajeti ya wizara hiyo kutoka Sh. Bilioni 89 hadi 231 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
“Bajeti hii kubwa tuliyopewa inakwenda kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa kama vile magari 89 na pikipiki 140 ambazo zitatumika kuyafikia maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini na ukusanyaji wa maduhuli.
Pia ametoa maagizo matano kwa maofisa madini wakazi wa mikoa kutatua kwa haraka migogoro ya wachimbaji wa madini kwa kusimamia haki.
Lingine ni kuimarisha udhibiti wa utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na vikosi kazi, vyombo vya ulinzi na usalama na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Maagizo mengine ni Ofisi ya Kamishna wa Madini kwa kushirikiana na Ofisi za Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa kushirikiana kwa pamoja kuwalea, kuwakuza na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema kupitia ushirikishwaji kwa watendaji wa wizara hiyo na taasisi zake, mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa umeendelea kukua.
Amesema uhakika upo ifikapo mwaka 2025 mchango huo kwenye pato la taifa utafikia asilimia 10.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Yahya Samamba amesema wizara na taasisi zake ipo tayari kufanyia kazi maelekezo mazuri yanayoendelea kutolewa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na rasilimali za madini nchini.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Buriani amesema sekta hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa cha ukusanyaji wa mapato ya mkoa.
Amealika wawekezaji kujitokeza katika mkoa kwa kuwa kuna wingi wa madini ya metali, ujenzi, vito na ya viwandani.
Pia ameomba wachimbaji wadogo na wakinamama kupewa mitaji na elimu kuhusu uchimbaji wa madini.