Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: MWENYEKITI wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Profesa Masoud Muruke ametembelea Ofisi za TSC Wilaya ya Morogoro na kuwapongeza watumishi wa Wilaya hiyo kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao katika kutoa huduma kwa walimu.
Amesema licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili ofisi hiyo, watumishi hao wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na uzalendo, hivyo kufanya walimu wa Wilaya hiyo kuendelea kupata huduma bora.
Pia amewataka watumishi hao kuendelea kutoa huduma bora kwa walimu ambao ni watumishi muhimu katika kuzalisha kada mbalimbali ambazo zinahitajika kwa maendeleo ya Taifa.
Kwa upande mwingine ameitaka Menejimenti ya TSC kuhakikisha inaendelea kuboresha mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa Ofisi zake za wilaya kwani zenyewe ndio shina la kuleta mafanikio katika utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Amesema ni vema kuimarisha Ofisi za Wilaya kwa kuwa, na mazingira mazuri ya kuhifadhia nyaraka ambapo wakati mwingine zinatumika katika utoaji wa maamuzi ya masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wa walimu.
“Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) inagusa sehemu kubwa ya utumishi wa walimu ikiwemo ajira, maendeleo ya walimu na inatoa maamuzi yanayohusu nidhamu za walimu, hivyo ni vyema tuhakikishe tunaweka mazingira mazuri ya ofisi hizi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,” amesema.
Naye Katibu wa TSC, Paulina Nkwama amewataka Watumishi wa Tume wilayani Morogoro kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma kwa walimu katika maeneo yote ya Wilaya hiyo yakiwemo maeneo ya pembezoni kama Mvuha na Matombo.
Amesema maeneo ya Mvuha na Matombo yako mbali na ofisi za TSC, hivyo ni vyema kwa watumishi wa Tume kuweka utaratibu wa kupangiana zamu ya kuwafikishia huduma walimu katika maeneo hayo.