Na Lucy Ngowi
RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya sh bilioni 2.1 kwa ajili ya kuwezesha usimikaji wa mfumo, miundombinu na vitendea kazi, kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa mashauri ya wafanyakazi kwa njia ya mtandao.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Protrobas Katambi amesema hayo, alipokuwa akifungua, Mafunzo ya Mfumo wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mashauri kwa Njia ya Mtandao (OCMS) kwa wadau.
“Ninyi wote ni mashahidi kwamba tumemsikia mara nyingi Rais Samia akisisitiza matumizi ya mifumo, na kwamba isomane ili kupunguza na ikibidi kuondoa urasimu katika utoaji wa huduma,”.

Katambi amesema na kuongeza kuwa utolewaji wa fedha hizo ni dhahiri amesikia maoni ya wafanyakazi yaliyotolewa siku kuu ya wafanyakazi (Mei Mosi).
Amesema mifumo hii itawafanya wananchi waweze kupata taarifa na kuhudumiwa kwa muda mfupi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ( CMA), Usekelege Mpulla amesema, wakati wa Maadhimisho ya Mei Mosi Kitaifa mwaka huu, upande wa wadau hususan waajiri na waajiriwa waliwasilisha hoja kuhusu mifumo ya utatuzi ya migogoro ya kazi nchini.
Amesema,” Na hoja kubwa ilikuwa ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, huduma zake hazipo kila mahali, serikali sikivu baada ya kusikia hilo, ilijibu kwa kuwasilisha na kuelezea kuhusu mkakati huu, ambao Rais Samia ndani ya muda mfupi ametenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba unatekelezeka,”.
Amesema mfumo huo ukianza kutumika utakuwa ni majibu kwa changamoto za muda mrefu za wananchi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Mpulla amesema, kabla ya kuanza kwa matumizi ya mfumo huo, tangu kuanzishwa kwa tume ya usuluhishi na uamuzi mwaka 2007, tume ilitatua migogoro ‘manual’.

“Tulikuwa tunatakiwa kupeleka majalada Mahakama Kuu na kumekuwa na malalamiko ya uchelewaji.
“Mfumo huu mpya, taarifa zake zitasomana na mahakama, zitasomana na Ofisi ya Kamishna wa Kazi kwa wafanyakazi ambao ni wageni wanaopata vibali kufanya kazi nchini,” amesema.
Pia amesema kupitia mfumo huo, wadau mbalimbali wataweza kuwasilisha mashauri bila ya kupanga foleni kwenye tume ya usuluhishi na uamuzi, ama kusafiri umbali mrefu.
Amesisitiza pia, kupitia mfumo huu, ufanisi katika tume hiyo utaongezeka, pia utatuzi wa migogoro ya kikazi utakwenda kwa haraka zaidi ya ilivyozoeleka.