Na Lucy Ngowi
OFISA Mfawidhi Dar es Salaam kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Yohana Massawe amesema endapo mwajiri hatakuwa tayari kumrudisha kazini mfanyakazi, sheria inamtaka kulipa fidia ya mishahara ya miezi 12.
Ikiwa ni pamoja na mishahara ambayo mfanyakazi hakulipwa tangu kuachishwa kazi mpaka siku ya kulipwa.
Massawe amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Mfanyakazi kuhusu namna CMA inavyoshughukikia migogoro ya kikazi.
Amesema katika hilo sheria itachukua mkondo wake kama upande wa utetezi utaonyesha mwajiriwa ana haki hiyo.
Amesema mbali na mwajiri kumlipa mfanyakazi miezi 12, anapaswa kumlipa mishahara kwa kipindi chote alichokuwa ameachishwa kazi , mpaka atakapolipwa na haki nyingine ambazo sheria inaainisha kwa mfanyakazi aliyeachishwa kazi.
“Kinachotakiwa wakati wanapatana yale mapatano yawe ya wazi kwamba kama wanarudi ni kwa utaratibu upi, na kama kuna stahiki wanazopaswa kupewa kwa kipindi walichokuwa nje, lazima makubaliano yawe wazi ” amesema.
Amesema inapotokea mfanyakazi hakurudishwa kama walivyokubaliana kinachotakiwa kufanywa ni kuomba utekelezaji, na anayefanya utekelezaji ni Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
“Kwa hiyo anatakiwa kuwasilisha maombi ya utekelezaji ya yale makubaliano mbele ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambao watachukua hatua kuhakikisha kila mtu anapata haki yake,” amesema.
Awali amesema makubaliano yàliyofikiwa baina ya mwajiri na mwajiriwa mbele ya CMA yasipotekelezeka, basi mshinda tuzo hupeleka mbele ya Màhakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa ajili ya maombi ya kukazia makubaliano hayo.