Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetangaza rasmi kuwa Novemba 27, 2024 itakuwa ni siku
ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara na upigaji wa kura utaanza saa mbili kamili asubuhi na kumalizika saa 10 kamili jioni.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Mohamed Mchengerwa amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kutolewa tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa Kwa mwaka 2024.
Amesema Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka
2019 anautangazia umma wa Watanzania na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu .
“Ninawatakia uchaguzi mwema, amani na utulivu katika kipindi chote cha uandikishaji, uteuzi wa wagombea, kampeni, upigaji kura, wakati wa kutangaza na kupokea matokeo ya uchaguzi,’amesema.
Amesema Uchaguzi huo unaongozwa na Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya vijiji, Vitongoji na mitaa katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka
za Miji.
Amesema Kwa mujibu wa Kanuni hio, uandikishaji na uandaaji wa Orodha ya wapiga kura utaanza siku ya 47 kabla ya siku ya uchaguzi na utafanyika kwa muda wa siku 10 kwa kutumia fomu iliyoainishwa katika Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi katika majengo ya umma na pale
ambapo hakuna jengo la umma,
Uandikishaji utafanyika kwenye sehemu ambayo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atakuwa amekubaliana na viongozi wa vyama vya siasa.
Amesema Kwa mujibu wa Kanuni hizo, vituo vya kujiandikisha kupiga kura na kupigia kura, kwa maeneo yaliyo chini ya Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo vitakuwa katika ngazi ya kitongoji.
Kadhalika amesema Kwa upande wa Mamlaka za Miji (Miji, Manispaa na Majiji), vituo vya kujiandikisha kupiga kura na kupigia
kura vitakuwa katika ngazi ya mtaa.