Na Lucy Ngowi
DODOMA: MAMLAKA ya Mimea na Viuatilifu nchini (TPHPA), ina mchango mkubwa wa nchi katika kuwa na utoshelevu wa chakula kutokana na jitihada inayofanya ya kudhibiti visumbufu vya mazao.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo wakati wa Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, yanayofikia kilele chake kesho.
Amesema katika siku za karibuni mamlaka hiyo ilifanikiwa kudhibiti ndege aina ya kwelea kwelea ambao walikuwa wakishambulia mashamba makubwa ya mpunga.
“Tunaona mamlaka ikidhibiti tija ikaongezeka inachangia kwenye ongezeko la chakula, pia inaimarisha masoko,” amesema.
Kwa upande mwingine amesema, mamlaka hiyo inapofanya kazi zake inachangia utekelezaji wa vipaumbele vya wizara ya kilimo.
“Kwa sasa hivi mamlaka imeandaa taarifa ambayo inasaidia kufunguka kwa masoko katika nchi 15. Hivi karibuni mabalozi watakabidhiwa taarifa hizo,” amesema.
Maelezo ya Profesa Ndunguru ni kwamba, mwisho wa siku mchango wa mamlaka utasaidia kuonekana katika kukua kwa pato la taifa.