Na Lucy Ngowi
DODOMA: VIJANA wameitiwa fursa ya mgahawa unaotembea ambao utawawezesha kuwapatia kipato kitakachowasaidia kuendesha maisha yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa nchini, Primus Kimaryo amesema hayo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yajulikanayo kama 88 yanayoendelea Jijini Dodoma.
Amesema kwa kutambua fursa hiyo kwa vijana, bodi imezindua mradi wa mgahawa unaotembea maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu ili kutoa huduma ya unywaji wa kahawa.
“Mkakati huu unalenga kuongeza unywaji wa kahawa kutoka asilimia saba mpaka nane ambao ni unywaji wa sasa kufikia asilimia 15,” amesema.
Amesema bodi imeona ifanye hivyo ili kuongezea thamani zao la kahawa ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa vijana.
Kwa maelezo ya Mkurugenzi Mkuu huyo, vijana watakaopata mradi huo kwa mkopo nafuu, ambao baada ya miaka mitatu mhusika anapaswa kurejesha gharama hizo kisha mgahawa huo unakuwa mali yake.
” Msukumo mkubwa ni kuona namna gani vijana wanaweza kupata ajira kupitia zao la kahawa kwani kijana kupata ardhi au kukodisha mgahawa ni changamoto,” amesema.
Aidha amesema,mpaka hivi sasa gharama za mkopo huo ni shilingi milioni 30 huku akisema wanaanza kwa kutengeneza migahawa 100 ambayo itatengenezwa kwa awamu.
Na kwamba vijana watakaokidhi vigezo vya kupata mkopo huo, watapatiwa mafunzo ya uendeshaji wa migahawa hiyo ili ilete tija iliyokusudiwa.