Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 7, 2026
Habari Author 1

TANESCO Yajenga Njia Mbadala Ya Umeme Kupunguza Changamoto Ya Umeme Mbagala,Kigamboni Mkuranga Na Kibiti

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA  la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikisha kwa haraka ujenzi wa njia nyingine ya muda ya kusafirisha umeme ya juu (overhead) ikiwa ni  juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wateja wa maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti, waliokumbwa na changamoto iliyojitokeza kwenye njia ya kusafirisha umeme chini ya ardhi yenye msongo wa kilovoti 132 (132kV) katika eneo la Gongolamboto.
Hatua hiyo imekuja baada ya wataalamu wa TANESCO kubuni na kuanza kutekeleza njia hiyo mbadala ya muda wa kusafirisha umeme kwa njia ya juu, unaovuka eneo la miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR), ili kufidia sehemu ya njia ya chini ya ardhi iliyopata hitilafu na kuhakikisha wateja wanaendelea kupata huduma ya umeme wakati matengenezo yakiendelea.
Habari Picha 14337
Habari Picha 14338
Akizungumza leo, tarehe 7 Novemba 2026, wakati wa akikagua maendeleo ya kazi za matengenezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,  Lazaro Twange, amepongeza jitihada za wataalamu wa Shirika kwa kujenga kwa haraka na kutekeleza suluhisho hilo la dharura ili kupunguza changamoto kwa wateja walioathirika.
Amesema TANESCO inaendelea kuchukua hatua za kiufundi kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa wateja wakati wote, huku kazi za kurekebisha miundombinu iliyoharibika zikiendelea.
“Tumefika hapa kukagua maendeleo ya kazi na kujionea hatua zinazochukuliwa na wataalamu wetu. Tumefarijika kuona kuwa wameweza kutengeneza njia nyingine mbadala ya juu inayovuka eneo la SGR ili kuhakikisha umeme unaendelea kusafirishwa na kuwafikia wateja wetu wakati matengenezo ya njia ya ardhini yakiendelea. Tunawahakikishia wateja wetu kuwa tunaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata huduma ya umeme,” amesema  Twange.
Habari Picha 14339
Habari Picha 14340
Aidha, amesisitiza kuwa TANESCO inaendelea kuimarisha miundombinu yake na kutafuta suluhisho zinazopunguza athari kwa wateja pale changamoto za kiufundi zinapojitokeza, akibainisha kuwa kuridhika kwa wateja na upatikanaji wa huduma ya uhakika ni kipaumbele cha Shirika.
Kwa upande wake, wataalamu wa TANESCO wameendelea na hatua za kuunganisha na kukamilisha mfumo huo mbadala, kazi inayohitaji tahadhari na kufanyika kwa kuzingatia taratibu za usalama ili kuhakikisha njia hiyo inakuwa tayari kutumika kwa ufanisi.
Hitilafu hiyo ilianza kujitokeza Novemba 3, 2026, katika njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 inayounganisha Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Gongolamboto na vituo vya Mbagala na Dege, Kigamboni.Ambapo Changamoto hiyo iliathiri upatikanaji wa umeme katika baadhi ya maeneo ya Mbagala, Kigamboni, Mkuranga na Kibiti kutokana na njia mbadala iliyokuwepo awali kuwa na uwezo mdogo wa kubeba mahitaji yote ya umeme kwa wakati mmoja.
Habari Picha 14341
Habari Picha 14342
Habari Picha 14343
TANESCO inaendelea na juhudi za kurekebisha miundombinu hiyo kwa lengo la kurejesha hali ya kawaida na kuimarisha uhakika wa huduma ya umeme kwa wateja wake.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.