Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 7, 2026
Habari Author 1

STAMICO Yatakiwa Kuongeza Uzalishaji Na Kufikia Kuwa Kinara Barani Afrika-Mavunde

Na Lucy Lyatuu,Dodoma

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amelitaka  Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha kipindi cha miaka mitafu ijayo  wanaongeza uzalishaji na uwekezaji katika miradi yao na kufikia kuwa  kiongozi katika bara la Afrika kwa kukuza na kuimarisha sekta ya madini.

Ameitaka STAMICO kutumia fursa za rasilimali za madini zilizopo nchini kupanua uwekezaji wake, kuongeza uzalishaji na kuimarisha mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Mavunde amesema hayo baada ya kuzindua kiwanda kikubwa  cha STAMICO  cha kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquette kilichojengwa eneo la  Msembeta kata ya Chigongwe jijini Dodoma.

Habari Picha 14324

Kiwanda hicho ni cha nne kwa shirika hilo tangu kuanza kwa uzalishaji wa bidhaa hiyo inayotokana na makaa ya mawe, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala kwa wananchi.

Viwanda vingine vimejengwa Kisarawe,Tabora na Kiwira na hicho cha Dodoma lengo likiwa ni kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kupunguza athari za mazingira hususani ukataji miti.

Amesema shirika hilo linapaswa kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika miradi mbalimbali ya madini, ikiwemo dhahabu eneo la Kigosi, madini ya kimkakati mkoani Morogoro na nikeli mkoani Mtwara, ili kuongeza wigo wa shughuli zake na kuimarisha mapato.

Habari Picha 14325

Kuhusu  mabadiliko ya shirika hilo, Mavunde amesema miaka mitano iliyopita STAMICO lilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyotathminiwa na kutakiwa  kufutwa kutokana na kutokuwa na tija, lakini kwa  sasa limefikia mapato ya zaidi ya Sh bilioni 89 kutoka Sh bilioni moja.

Alisema anataka STAMICO kuwa shirika kinara katika kukuza mchango wake kwemye madini na kuwa mshindani hata kwa mashirika makubwa.

Kuhusu mkaa, Mavunde amesema mkaa wa Rafiki Briquette una uwezo wa kuwaka kwa zaidi ya saa tatu na nusu, huku kilo moja ikiuzwa kwa Sh1,000.

Amelitaka shirika hilo kuhakikisha bidhaa hiyo inasambazwa kwa wingi na kupatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali nchini, badala ya kubaki katika maeneo yanayozalishwa pekee.

Habari Picha 14326

Amesisitiza umuhimu wa STAMICO kuimarisha mfumo wa masoko kwa kushirikiana na wafanyabiashara na mawakala, akieleza kuwa uzalishaji unapaswa kwenda sambamba na mikakati madhubuti ya kuwafikia watumiaji.

“Matumizi ya nishati hiyo ni sehemu ya mchango wa sekta ya madini katika kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” Amesema Waziri Mavunde.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesema kiwanda cha Dodoma kimejengwa kwa kuzingatia nafasi ya mji huo kama makao makuu ya nchi pamoja na mahitaji ya nishati safi katika mkoa huo na maeneo jirani.

Habari Picha 14327

Amesema Shirika limejenga mtandao wa mawakala 92 nchini, wakiwemo 35 kutoka taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania, kwa lengo la kurahisisha usambazaji wa bidhaa hiyo kwa wananchi.

“Katika uzinduzi wa kiwanda hiki kikundi hicho kimekabidhiwa  magari madogo aina ya toyo 30 na makontena kwa ajili ya kuwezesha usafirishaji na uuzaji wa Rafiki Briquette katika maeneo mbalimbali, ” Amesema

Dkt. Mwasse amesema wazo la kuzalisha bidhaa hiyo lilitokana na utafiti ulioanza mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2022, huku bidhaa hiyo ikipata cheti cha ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Habari Picha 14328

“STAMICO inaendelea na maandalizi ya kujenga kiwanda kingine mkoani Geita ili kuongeza uzalishaji na kusogeza huduma karibu na wananchi,” amesema na kuongeza kuwa mbali na uwekezaji katika nishati ya kupikia, amesema shirika hilo limeagiza mitambo 10 ya uchorongaji madini kwa lengo la kuimarisha shughuli za utafiti na kuongeza ajira kwa vijana.

Ameeleza kuwa kila mtambo mmoja unatarajiwa kutoa ajira kwa vijana takribani 30, hivyo mitambo yote ikianza kufanya kazi itatoa fursa za ajira kwa vijana takribani 300.

Naye mwakilishi wa taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania Fatuma Madidi amesema wanawake wamepata fursa ya kuwa mawakala wa bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini na wamejipanga kuhakikisha inawafikia watumiaji wengi zaidi.

Habari Picha 14329
Habari Picha 14330
Habari Picha 14331
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.