Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Author 3

Spika Wa Bunge Ataka Mafanikio Ya Bunifu Nchini Yapimwe Kwa Uwezo Wa Kutumika Katika Jamii

Na Lucy Lyatuu,Dodoma
SPIKA  wa Bunge, La Jamhuri Ya Muungano Tanzania Mussa Aźzan Zungu, amesema bunifu  zilizopo nchini zinaonesha  uwezo wa vijana na watafiti wa Kitanzania katika kutumia sayansi na teknolojia kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.
Hata hivyo, amesema  mafanikio ya bunifu hizo hayatapimwa kwa kuoneshwa kwenye maonesho pekee, bali kwa uwezo wake wa kuzalishwa, kupata wateja na kutumika katika jamii.
Akizungumza wakati wa kuonesha baadhi ya bunifu zilizotokana na taasisi za elimu ya juu nchini katika viwanja vya Bunge, Zungu amesema  ipo haja ya Serikali  kuunganisha tafiti na mahitaji halisi ya jamii, ili bunifu zisibaki kwenye makaratasi au maonesho pekee.
Amesema taasisi za Serikali na sekta binafsi zinapaswa kuangalia uwezekano wa kutumia  bidhaa zinazozalishwa na wabunifu wa ndani, ili kuwapa uhakika wa soko na kuwahamasisha kuendelea kubuni teknolojia nyingine.
Zungu amesema pia ni muhimu kufuatilia matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kusaidia wabunifu, akitaka kufahamu namna fedha hizo zinavyowanufaisha wabunifu na matokeo yanayopatikana.
Amesema   vijana wanahitaji kupewa fursa ya kuonesha uwezo wao, kupata usaidizi wa kifedha na kuunganishwa na taasisi zinazoweza kuzalisha bunifu zao kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake Waziri Wa Elimu Sayansi Na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema serikali  itaongeza juhudi za kuwawezesha vijana wa Kitanzania kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kutatua changamoto za jamii.
Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha bunifu zilizokomaa zinafanyiwa tathmini, zinazalishwa viwandani na kuingizwa sokoni ili kutoa ajira na kuchochea uchumi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya sayansi na teknolojia kwa lengo la kujenga uwezo wa watafiti na wabunifu wa ndani, pamoja na kuweka mazingira yatakayowawezesha kubadili mawazo yao kuwa bidhaa zinazoweza kutumika na wananchi.
Ametaja ubunifu wa mkanda maalumu unaolenga kusaidia kupunguza kutokwa na damu nyingi kwa wanawake baada ya kujifungua, ambao umetengenezwa na wabunifu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya.
Amesema kwa mujibu wa maelezo aliyoyapata, teknolojia hiyo imefanyiwa utafiti na majaribio, huku hatua za kuanzisha uzalishaji wake zikiendelea kupitia kiwanda kilichoanzishwa kwa ajili ya kutengeneza bidhaa hiyo.
Amesema ubunifu mwingine ni wa teknolojia ya kutenganisha maji na kupata gesi ya oksijeni na hidrojeni, uliofanywa na mbunifu Luvanda kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya.
“Teknolojia hiyo inaweza kuwa na matumizi mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa oksijeni kwa matumizi ya kitabibu na hidrojeni kama chanzo cha nishati, ikiwemo matumizi ya kupikia,” amesema.
Hata hivyo, amesema ameelekeza Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kushirikiana na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji, ufanisi na usalama wa teknolojia hiyo kabla ya kuendelezwa kwa matumizi mapana.
 Prof Mkenda amesema ameona bidhaa za ngozi zilizotengenezwa na mbunifu aliyepata mafunzo ya uzamivu katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, iliyopo Arusha.
Amesema ubunifu huo unaonesha uwezekano wa kutumia mabaki ya maganda ya korosho kama malighafi katika kutengeneza kemikali zinazotumika katika usindikaji wa ngozi, hatua inayoweza kuongeza thamani ya mazao ya korosho na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Ameeleza kuwa mazungumzo yanaendelea kati ya taasisi husika na mbunifu huyo ili kuona namna ya kusaidia kuanzishwa kwa kiwanda cha kuzalisha bidhaa hizo, ikiwemo katika Mkoa wa Dar es Salaam
Profesa  Mkenda pia ametaja ubunifu wa teknolojia inayolenga kuzalisha saruji kwa kutumia nishati kidogo, huku ikilenga kuboresha ubora na kupunguza gharama za uzalishaji.
Aidha, ameonesha ubunifu wa mita ya umeme inayoweza kuruhusu wapangaji kadhaa kutumia mita moja kuu lakini kila mpangaji akawa na mfumo wake wa kulipia na kufuatilia matumizi ya umeme.
“Teknolojia hiyo inaweza kusaidia kupunguza migogoro inayotokea katika nyumba za kupanga kutokana na kutokuelewana kuhusu kiasi cha umeme kinachotumiwa na kila mpangaji,” amesema.
Aidha amesema  anatarajia kufanya mazungumzo na wazalishaji pamoja na wadau wa sekta ya nishati, ikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ili kutathmini uwezekano wa teknolojia hiyo kuzalishwa na kutumika kwa upana zaidi.
Amesema pamoja na kuendelea kuunga mkono tafiti na bunifu, hatua muhimu inayofuata ni kuhakikisha bidhaa hizo zinapata soko na zinanunuliwa na taasisi za Serikali pamoja na sekta binafsi.
Amesema Serikali ina wajibu wa kushirikiana na wabunifu ili kuwasaidia kupata mitaji, teknolojia na fursa za uzalishaji, huku akieleza kuwa uwekezaji unaofanyika katika sayansi na teknolojia unalenga kuleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
Ametaja hatua mbalimbali za Serikali katika kuendeleza sekta hiyo, ikiwemo ufadhili wa masomo, kuimarisha shule za sayansi, kutoa tuzo kwa wahadhiri na watafiti pamoja na kuweka mifumo ya kusaidia wabunifu kuendeleza bidhaa zao hadi kufikia hatua ya kuingia sokoni.
 Mbunge wa Msalala na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mabula Magangila, amepongeza uwekezaji wa Serikali katika sayansi na teknolojia, akisema umeanza kuonesha matokeo kupitia bunifu mbalimbali zinazotokana na taasisi za elimu ya juu nchini.
Amesema miongoni mwa bunifu alizoziona ni mashine za teknolojia ya CNC zinazoweza kutumika katika shughuli za uhandisi na viwanda, ikiwemo kukata na kutengeneza maumbo mbalimbali kwa usahihi.
Aidha, amesema ubunifu wa kutumia maganda ya korosho kutengeneza kemikali zinazotumika katika usindikaji wa ngozi ni hatua inayoweza kusaidia kupunguza matumizi ya kemikali zisizo rafiki kwa mazingira na kuongeza thamani ya mabaki ya mazao ya kilimo.
Amesisitiza kuwa tafiti zinazofanywa na Watanzania zinapaswa kuendelezwa hadi kuwa bidhaa zinazoweza kutatua changamoto za wananchi, kuongeza uzalishaji na kufungua fursa za ajira.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.