Na Mwandishi Wetu
UPATIKANAJI wa mikopo kwa kaya maskini unaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ufanisi wa juhudi za kupambana na umaskini nchini, utafiti umebaini.
Matokeo hayo ni miongoni mwa tafiti kumi zilizowasilishwa na watafiti waliofadhiliwa na Mfuko wa DEEP Challenge Fund katika warsha iliyowakutanisha watafiti, watunga sera na washirika wa maendeleo jijini Dodoma, Oktoba 21, 2026.
Utafiti ulioongozwa na Profesa Esther Ishengoma umebaini kuwa mabadiliko ya viwango vya joto yana uhusiano mkubwa na umaskini, huku upatikanaji wa mikopo ukitajwa kusaidia kupunguza athari hizo kwa kaya.

Watafiti wa mfuko wa DEEP Challenge Fund wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa warsha ya kusambaza matokeo ya tafiti zao iliyofanyika Dodoma, tarehe 21 Oktoba 2026.
Katika utafiti mwingine, Dkt. Peter Binyaruka amebaini kuwa kaya maskini zina uwezekano mdogo wa kutafuta huduma za afya na mkubwa wa kukabiliwa na gharama za matibabu zinazoweza kudhoofisha hali yao ya kifedha.
Utafiti huo pia umeonesha kuwa rasilimali za afya zimejikita zaidi katika mikoa yenye hali nzuri ya kiuchumi, huku tofauti za matumizi ya huduma hizo kati ya mikoa tajiri na maskini zikiendelea kuongezeka.
Kwa upande wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF/PSSN), Dkt. Cornel Joseph na wenzake wamebaini kuwa mpango huo unawafikia watu walio katika mazingira magumu, lakini kuboresha utendaji na kupanua aina za msaada kunaweza kuongeza mafanikio yake katika kupunguza umaskini.

Matokeo mengine yameonesha kuwa haki salama za umiliki wa ardhi zina mchango mdogo katika kupunguza umaskini wa kaya zisipoambatana na upatikanaji wa mikopo.
Akizungumza katika warsha hiyo, Dkt. Charles Sokile, Mkurugenzi Mkazi wa Oxford Policy Management nchini Tanzania, amewahimiza watunga sera kutumia ushahidi wa tafiti hizo katika kupanga na kufanya maamuzi ya kukabiliana na umaskini uliokithiri.
Mfuko wa DEEP Challenge Fund hufadhili tafiti zinazoongozwa na watafiti wa ndani ili kuziba mapengo ya ushahidi na kusaidia kupata suluhisho la changamoto za umaskini.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!