Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 5, 2026
Habari Lucy Ngowi 11

SOS Yageuza Changamoto Za Vijana Kuwa Fursa Za Ujasiriamali

Na Lucy Ngowi

RUKWA: VIJANA wanaokabiliwa na changamoto za kifamilia na kijamii wanajengewa uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali, ujuzi wa kuendesha biashara na utengenezaji wa bidhaa zinazoweza kuwaingizia kipato, kupitia SOS Children’s Villages Tanzania.

Hatua hiyo inalenga kuwasaidia vijana walio katika mazingira magumu, wakiwemo waliopoteza malezi ya familia na waliokatiza masomo kutokana na changamoto mbalimbali, kupata ujuzi na fursa za kujenga maisha yao.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani Rukwa, Ofisa Vijana wa SOS Children’s Villages Tanzania, Philip Namanga, amesema shirika hilo linashirikiana na familia, Serikali na wadau mbalimbali kuwawezesha vijana kujitambua, kutumia vipaji vyao na kujikwamua kiuchumi.

Habari Picha 14055

Amesema vijana wanaonufaika na programu hizo hujengewa uwezo wa kuanzisha na kuendesha biashara, kutengeneza bidhaa na kuzitangaza kwa wateja, hatua inayowasaidia kutumia ujuzi wao kujipatia kipato.

Namanga amesema ushiriki wa shirika hilo katika maonesho hayo ni fursa ya kuonesha bidhaa zinazotengenezwa na vijana pamoja na uwezo wao wa kutumia ujasiriamali kujenga maisha bora.

Ameeleza kuwa ushirikiano na wadau ni muhimu katika kuwajengea vijana kujiamini, kutambua fursa zinazowazunguka na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Habari Picha 14056

Kuhusu ulinzi na malezi ya watoto, amesema SOS Children’s Villages Tanzania hushirikiana na idara za ustawi wa jamii kuwasaidia watoto wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali, wakiwemo waliopoteza familia, waliopitia ukatili na wanaohitaji uangalizi maalumu.

Amesema pale inapowezekana na kuwa katika maslahi ya mtoto, shirika hushirikiana na familia kuboresha mazingira ya malezi, huku likisisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na huduma wanazohitaji.

Namanga ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na taasisi zinazosaidia watoto na vijana walio katika mazingira magumu ili kuwajengea uwezo, kuimarisha malezi na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.