Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 20

GEWOMA: Leseni Tatu Zafungua Fursa Kwa Wachimbaji Geita

Na Lucy Ngowi
GEITA: WACHIMBAJI wadogo wa madini ya dhahabu mkoani Geita wamefunguliwa fursa mpya baada ya kukabidhiwa leseni tatu za uchimbaji zinazohusisha eneo la takribani ekari 60, hatua inayowawezesha kufanya shughuli zao kwa utaratibu unaotambulika kisheria.
Leseni hizo zimekabidhiwa kwa wachimbaji hao wakati wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kwa leseni hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Geita (GEWOMA), Asia Masimba, amesema hatua hiyo ni muhimu kwa wachimbaji wadogo waliokuwa wakihitaji maeneo rasmi ya kufanyia shughuli zao.
Masimba amesema kupatikana kwa leseni hizo kumeongeza matumaini kwa wachimbaji hao kuanza maandalizi ya uchimbaji na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini.
Amesema wachimbaji hao wameishukuru Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Geita na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata leseni hizo, wakieleza utayari wa kuanza shughuli za uchimbaji baada ya kukamilika kwa maonesho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa katika tukio hilo, leseni hizo tatu zinahusisha eneo la takribani ekari 60, huku wachimbaji wakitarajiwa kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji wa dhahabu na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.