Na Lucy Ngowi
GEITA: KAMPUNI ya ESAP Mining Services Limited imeibuka na ushindi wa tuzo tatu katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, ikitaja mafanikio hayo kuwa chachu ya kuendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji.
Kampuni hiyo ilitwaa tuzo ya Mdhamini Mkuu wa Maonesho, Kampuni Bora ya Uchorongaji Miamba (Drilling) na kushika nafasi ya pili katika kipengele cha Kampuni Bora ya Uchimbaji Madini.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hizo katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita, Ofisa Utawala na Mawasiliano wa ESAP Mining Services Limited, Shabani Mitenenko Sadiki, amesema kutambuliwa huko kunaipa kampuni hiyo msukumo wa kuendelea kuboresha huduma na kutumia teknolojia zinazoongeza tija katika sekta ya madini.
Amesema tuzo hizo ni sehemu ya matokeo ya juhudi za kampuni katika kubuni na kutumia mbinu za kisasa zinazolenga kuongeza ufanisi katika huduma za uchimbaji inazozitoa kwa wadau mbalimbali.
“Tunatambua tuzo hizi kama hamasa ya kuendelea kuboresha huduma zetu, kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza ubunifu katika shughuli za uchimbaji,” amesema Sadiki.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuweka sera, sheria na kanuni zinazohimiza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi kupitia Local Content, akisema hatua hiyo imefungua fursa kwa kampuni za ndani kushiriki zaidi katika sekta ya madini.
Amesema ushiriki huo unaiwezesha kampuni za Kitanzania kutoa huduma kwa wawekezaji na wadau wengine wa sekta ya madini, hatua inayoongeza fursa za biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Sadiki pia amewashukuru viongozi na wafanyakazi wa ESAP Mining Services Limited kwa mchango wao ulioiwezesha kampuni hiyo kupata mafanikio hayo, pamoja na wadau wanaoshirikiana nayo katika shughuli za uchimbaji.
Amezitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa Nyanzaga, Buckreef, Stamigold na Shanta Mining, pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya kampuni zinazotoa huduma za uchimbaji, wawekezaji na wachimbaji wadogo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa shughuli za madini na kupanua fursa kwa kampuni za Kitanzania.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!