Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 17

DIB Yaeleza Mchango Wake Katika Kuimarisha Uthabiti Wa Sekta Ya Benki

Na Lucy Ngowi

GEITA: BODI ya Bima ya Amana (DIB) imewataka wananchi kuachana na tabia ya kuhifadhi fedha majumbani, ikieleza kuwa fedha hizo hazishiriki kikamilifu katika mzunguko wa uchumi na zinaweza pia kuwaweka wamiliki na familia zao katika hatari ya kupoteza mali zao.

Meneja wa Fedha na Uhasibu wa DIB, Romuli Mtui, amesema hayo wakati wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita.

Mtui amesema fedha zinapowekwa benki, zinaweza kutumika na watu wengine kupitia mikopo kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo.

“Fedha zinapowekwa nyumbani haziji kwenye mzunguko wa uchumi, lakini zikiwa benki, watu wanaozihitaji wanaweza kuzikopa na kuziendesha kwa shughuli mbalimbali za maendeleo,” amesema.

Amesema mbali na kutoshiriki kikamilifu katika mzunguko wa uchumi, fedha zinazohifadhiwa nyumbani ziko katika hatari ya kuibwa au kuharibiwa na majanga kama moto na mafuriko.

Mtui ametumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kuhusu Bima ya Amana, akisema huduma hiyo inawalinda wawekaji bila wao kulipa ada au kujisajili moja kwa moja.

Amesema mwananchi anachotakiwa kufanya ni kutumia huduma za benki au taasisi ya fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kwa kufanya hivyo anakuwa mnufaika wa mfumo wa bima ya amana endapo taasisi anayohifadhi fedha itashindwa kuendelea na shughuli zake.

“Bima yetu ya amana ni tofauti kwa sababu mwananchi hakatiwi kuchangia chochote wala hatakiwi kujisajili.

Anachopaswa kufanya ni kutumia huduma za kibenki katika benki au taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania,” amesema.

Mtui amesema Mfuko wa Bima ya Amana ulianzishwa mwaka 1999 kwa mtaji wa Serikali wa takribani Sh. Bilioni 1.05 na tangu wakati huo umeendelea kuimarishwa kupitia michango ya benki na taasisi za fedha wanachama.

Kwa mujibu wake, kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, benki na taasisi za fedha zinatakiwa kuchangia mfuko huo, huku fedha hizo zikiwekezwa katika hati fungani za Serikali na vitega uchumi vingine ili kuukuza mfuko.

Amesema DIB pia hushiriki katika hatua za kushughulikia changamoto za benki au taasisi za fedha zinazoyumba, kabla hazijafikia hatua ya kufilisika, kwa lengo la kulinda maslahi ya wawekaji na kupunguza athari kwa mfuko.

“Lengo ni kuhakikisha wateja wanalindwa mapema na kupunguza uwezekano wa mfuko kutumia fedha nyingi kulipa fidia pale taasisi inaposhindwa kuendelea na shughuli zake,” amesema.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.