Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 5, 2026
Habari Lucy Ngowi 15

Dkt. Nungu: Taasisi Zisipoteze Maarifa Kwa Kuhama Kwa Watumishi

Na Mwandishi Wetu
WINDHOEK, NAMIBIA: TAASISI za utafiti barani Afrika zimetakiwa kuweka mifumo ya kuhifadhi ujuzi na uzoefu wa watumishi ili mabadiliko ya wafanyakazi yasiathiri utekelezaji wa majukumu na maendeleo ya taasisi hizo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, akisema fedha za utafiti pekee hazitoshi bila kujenga uwezo wa watu na mifumo itakayohakikisha maarifa yanabaki ndani ya taasisi.
Dkt. Nungu ametoa kauli hiyo katika mkutano wa Mpango wa Mabaraza ya Ufadhili wa Sayansi (SGCI) mjini Windhoek, Namibia, unaozikutanisha taasisi za Afrika zinazofadhili na kuratibu tafiti.
Habari Picha 13916
Amesema taasisi zinapaswa kuwa na watumishi wenye uwezo wa kubuni programu za utafiti, kutathmini maombi kwa uadilifu, kusimamia miradi na kueleza namna matokeo ya tafiti yanavyoweza kusaidia serikali na jamii.
“Uzoefu unaopatikana kazini unapaswa kuhifadhiwa ndani ya taasisi ili watumishi wapya waweze kuendeleza kazi iliyofanywa badala ya kuanza upya kila mtumishi mwenye uzoefu anapohama,” amesema.
Dkt. Nungu, anayeongoza eneo la kuimarisha uwezo wa taasisi katika awamu ya tatu ya SGCI, amesema uwezo huo ni muhimu katika kukabiliana kwa pamoja na changamoto za afya, usalama wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia.
Habari Picha 13915
Awamu hiyo ya miaka mitano, kuanzia 2026 hadi 2030, ina ahadi ya dola za Canada milioni 57, sawa na takribani dola za Marekani milioni 42, kwa shughuli za SGCI katika nchi zinazoshiriki.
Amesema mafanikio ya mpango huo yanapaswa kuonekana katika uwezo wa taasisi kuendesha programu bora za utafiti, kuwafikia watafiti wengi zaidi na kutumia matokeo ya tafiti katika maamuzi yenye manufaa kwa wananchi.
COSTECH ni mwanachama wa SGCI kwa upande wa Tanzania.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.