Na Lucy Lyatuu
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetumia jukwaa la Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuhamasisha Watanzania kulinda misitu, ukisisitiza kuwa rasilimali hiyo ndiyo msingi wa uhifadhi wa mazingira, uchumi na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Ujumbe huo ulitolewa katika Programu ya Mazingira iliyofanyika ndani ya maonesho hayo, ambapo taasisi mbalimbali zilitoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Akiwasilisha mada kuhusu Misitu na Mazingira, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Fandey Mashimba, amesema Tanzania ina takribani asilimia 55 ya eneo lake likiwa limefunikwa na misitu, rasilimali ambayo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
“Msitu ni kama moyo wa maisha yetu. Hivyo, wananchi, taasisi na jamii kwa ujumla tunapaswa kuhakikisha tunailinda na kuihifadhi kwa wivu mkubwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho pamoja na viumbe wengine wanaoutegemea,” amesema Mashimba.
Ameeleza kuwa misitu ina mchango mkubwa katika kuhifadhi vyanzo vya maji, bioanuwai, kufyonza hewa za gesijoto na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, huku ikitoa malighafi zinazochochea viwanda, biashara na ajira kupitia uchakataji wa mazao ya misitu.
Mashimba amesema matumizi endelevu ya mazao ya misitu yanaweza kuongeza thamani ya bidhaa, kuinua kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa bila kuharibu mazingira.
Akifungua programu hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kulinda mazingira, akieleza kuwa mafanikio ya juhudi za uhifadhi yanategemea ushiriki wa kila mmoja.
Mbali na mada ya TFS, washiriki walipata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, utunzaji wa mazingira na dhana ya uchumi mzunguko, ambapo ilielezwa kuwa taka zinaweza kubadilishwa kuwa bidhaa mpya, ajira na chanzo cha kipato badala ya kuwa mzigo wa mazingira.
Kupitia ushiriki wake katika programu hiyo, TFS imeendelea kuimarisha kampeni za uelimishaji wa umma kuhusu usimamizi endelevu wa misitu, kuhamasisha upandaji miti sahihi kwenye maeneo sahihi ili kuepusha matumizi ya miti ambayo huweza kuwa vamizi hivyo kuathiri mifumo ya ikolojia na kutishia maisha ya viumbe vinavyo tegemea misitu kama makazi. Aidha, ilisisitizwa umuhimu wa matumizi sahihi ya rasilimali za misitu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira kama ilivyo elekezwa kwenye malengo 17 ya Milenia.

