Na Lucy Lyatuu
MFUKO wa udhamini wa pembejeo za kilimo nchini, umeahidi kutekeleza dira ya Taifa ya maendeleo 2050 kwa kasi kwa kuhakikisha wakulima wengi wanaendelea kunufaika na mfuko huo ikiwemo kuwezeshwa katika mikopo ya bei nafuu ili kuwawezesha kujikita na kunufaika na kazi zao.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Mwanahiba Mzee katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Amesema taasisi yake imejipanga kuendana na Kasi ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuelekea utekelezaji wa dira2050.
“Mwaka huu wa fedha ambao tumeanza nao, sisi tumejipanga kuendana na kasi ya Rais na ukiwa ni mwaka wa kwanza wa utekeleza dira ya 2050, hii ni sehemu ya kwanza, sisi tumejipanga kwenda kufanya mahusiano au mashirikiano na taasisi za fedha ili mikopo ipatikane kwa Kasi na ipatikane kwa wingi kwa Tanzania nzima, ili wakulima wetu wasipate shida kupata mikopo ya bei na masharti nafuu ambapo itawaweza kulima kwa tija ili kuongeza kipato chao, kipato cha taifa, kuongeza ajira.
Tumejipanga kuwasilisha au kutekeleza mpango wa mwaka wa kwanza wa dira ya Taifa kwenye upande wa kilimo ikuhusiana na ajira na hasa kwa vijana na wanawake ambapo Rais anataka kuwekeza zaidi huko kwa sababu ndio nguvu kubwa ya Taifa.

