Na Lucy Ngowi
KAHAWA ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tanzania kupitia mauzo ya nje na kipato cha wakulima.
Hata hivyo, mafanikio ya zao hilo yanaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, mojawapo ikiwa ni mashambulizi ya wadudu waharibifu.

Miongoni mwa wadudu hao, ruhuka ametajwa kuwa adui mkubwa wa zao la kahawa duniani.
Kwa mujibu wa Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia Kituo cha Utafiti wa Kahawa cha TaCRI Lyamungu, Dkt. Godsteven Maro, ruhuka ni mdudu anayeshambulia punje za kahawa kwa kutoboa matunda na kuingia ndani ya punje.
Kitendo hicho huharibu ubora wa kahawa na kupunguza thamani yake sokoni, hivyo kuwaingizia wakulima hasara kubwa.
Dkt. Maro anazungumza hayo katika Maonesho ya 50 ya Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Anasema mdudu huyo si tatizo la Tanzania pekee, bali ni changamoto inayowakabili wazalishaji wa kahawa duniani.
Nchi kama Colombia zimekuwa zikiwekeza katika tafiti za kudhibiti ruhuka kwa kutumia mitego maalumu ya kumvutia na kumtega.
Kutokana na uzoefu huo, watafiti wa TaCRI wameboresha teknolojia hiyo ili iendane na mazingira ya Tanzania.
Mtego huo umetengenezwa kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi, huku ukitumia vimiminika kama spiriti au pombe za kienyeji kuvutia wadudu hao.
Kwa mujibu wa watafiti, mtego mmoja unaweza kunasa hadi wadudu ruhuka 600 kwa kipindi cha wiki moja.
Hii inaonyesha kuwa teknolojia hiyo inaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya wadudu wanaoshambulia mashamba ya kahawa ikiwa wakulima wataitumia kwa usahihi.
Faida nyingine ya mtego huo ni kwamba ni wa gharama nafuu na unaweza kutengenezwa na mkulima mwenyewe bila kuhitaji vifaa vya gharama kubwa.
Hali hiyo inaufanya kuwa suluhisho linalofaa kwa wakulima wadogo na wakubwa.
Kwa sasa, ruhuka ameendelea kuongezeka katika mashamba ya kahawa aina ya Arabica na Robusta nchini Tanzania.
Wataalamu wanaonya kuwa bila kuchukua hatua za haraka, mdudu huyo anaweza kuendelea kupunguza uzalishaji na ubora wa kahawa ya Tanzania.
Dalili za mashambulizi ya ruhuka ni pamoja na kuwepo kwa tundu moja au zaidi kwenye kitovu cha tunda la kahawa, iwe tunda bado ni bichi au limeiva.
Wakulima wanashauriwa kukagua mashamba yao mara kwa mara ili kubaini dalili hizo mapema na kuanza kutumia mbinu za udhibiti kabla uharibifu haujaongezeka.
Mbali na matumizi ya mitego, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kutumia mbinu za udhibiti husishi wa wadudu, ikiwa ni pamoja na usafi wa shamba, kuvuna kwa wakati, kuondoa matunda yaliyoshambuliwa na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo.
Kadiri sekta ya kahawa inavyoendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, matumizi ya teknolojia rahisi na bunifu kama huu wa TaCRI yanaweza kuwa suluhisho muhimu katika kupunguza hasara zinazotokana na wadudu waharibifu na kuongeza uzalishaji wa kahawa yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la dunia.

