Na Lucy Lyatuu, Dodoma
KATIKA siku 100 tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, serikali imetenga Sh bilioni tano kwa ajili ya kusaidia kampuni changa 50 za TEHAMA kupitia mikopo yenye riba nafuu itakayotolewa na benki za biashara.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ajira, kukuza bunifu na kuchochea ukuaji wa biashara zinazoendeshwa na vijana.
Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Angellah Kairuki amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za siku 100 zilizotolewa na Rais Dkt Samia .
Amesema sekta ya TEHAMA ni mhimili wa maendeleo ya Taifa kwa kuwa inagusa sekta zote, na ndiyo msingi wa mapinduzi ya kidijitali yanayolenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kidijitali unaoendeshwa na teknolojia.
Waziri Kairuki amesema kati ya ahadi 13 zilizotolewa na Rais Dkt Samia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ahadi tatu ziligusa moja kwa moja Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, na zote zimeanza kutekelezwa ndani ya muda uliopangwa, hatua iliyoongeza imani ya wananchi kwa uongozi wa Rais Samia katika kipindi cha awamu ya pili.
Kuhusu fedha hizo amesema zitawezesha utekelezaji wa ahadi ya upatikanaji wa mitaji kwa kampuni changa, kupata mitaji, kufanya biashara ndogondogo na hata kupanua wigo wa ajira.
” Rais Dkt Samia aliahidi uendeshaji wa biashara ndogondogo za kidigitali na ametekeleza ahadi hiyo ambapo hadi kufikia Januari mwaka huu 2026 tayari fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kampuni changa ziweze kupata mitaji na watakaokidhi vigezo ndio watakaopewa, ” Amesema.
Amesema mikopo hiyo inalenga ubunifu katika maeneo masuala ya fedha, kupanga matukio, afya, akili unde, kilimo, bima, elimu, lojistiki na katika lishe.
Waziri Kairuki amesema kwa sasa Wizara inakubaliana na benki ili kutoa mikopo kwa watakaokidhi vigezo ambapo zitaboresha huduma na kufungua fursa ikiwemo ya kuajiri watu takriban saba hadi 10 na kuongeza kipato na kuboresha hali za maisha huku serikali ikiongeza kipato pia.
“Ninatoa wito kwa vijana wabunifu kutumia fursa hiyo pindi ikitangazwa kutuma maombi ili waweze kukuza bunifu zao na kujipatia kipato, ” Amesema Kairuki na kuongeza kuwa tangazo litatolewa kupitia tovuti ya Wizara na katika vyama vyao kuanzianFebruari 11,2026.
Aidha amesema ndani ya siku 100, Wizara imeanza taratibu za kuanzisha Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA pamoja na kukamilisha rasimu ya Sera ya Kampuni Changa ya Mwaka 2026, inayolenga kuweka mazingira rafiki ya biashara, kuongeza upatikanaji wa mitaji, kuvutia uwekezaji na kukuza ajira kwa vijana nchini.

