Na Lucy Lyatuu, Dodoma
KATIKA kipindi cha siku 100 tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Wizara ya Madini imepiga hatua kubwa katila kuleta mchango mkubwa wa ongezeko katila pato la uchumi wa nchi kutoka adilimia 10 na kufikia asilimia 12.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema yapo mafanikio katika myanja mbalimbali ndani ya Sekta ya Madini katika kipindi hicho ambapo Sekta hiyo imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 311 ambayo sawa na asilimia 103.
Waziri Mavunde amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio mbalimbali katika Sekta ya Madini nchini.
Amesema Sekta hiyo inakuwa siku hadi siku ambapo uongezaji thamani kwenye madini zipo hatua kadha wa kadha ambazo zimechukuliwa.
“Kupitia Sera ya Madini ya Mwaka 2009, ndani ya siku 100 Sekta ya Madini imefanikiwa kutekeleza sera ya uongezaji thamani madini ikiwa pamoja na uendelezaji wa ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani na usafishaji wa dhahabu katika maeneo mbalimbali nchini,” Amesema na kuongeza kuwa mbapo mpaka sasa mkoa wa Dodoma una jumla ya viwanda tisa vya uongezaji thamani na viwanda vya vinne vya madini ya metali kama vile Shaba na nikeli.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imefanikiwa kujenga kiwanda cha kusafisha madini ya chumvi kitakacho hudumia mikoa ya Lindi na Mtwara ambacho tayari kimekamilika kwa asilimia 99.
Aidha amesema ndani ya Januari ma Februari, 2026 Wizara inatarajia kuwasha kwa majaribio kiwanda kikubwa cha kuyeyusha madini kilichopo jijini hapo.
Kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika mnyororo wa thamani madini, Waziri Mavunde ameeleza kuwa Sekta ya Madini imefanikiwa kuajiri jumla ya watanzania 18,000 katika ajira za moja kwa moja huku zaidi ya watanzania 6,000,000 wakijihusisha na shughuli mbalimbali za mnyororo wa thamani madini.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa, awali migodi ilikuwa ikitumia kiasi cha Sh trillion tano katika manunuzi nje ya nchi, lakini kutokana na mabadiliko ya Sheria na Kanuni, Sekta ya Madini imefanikiwa kuwezesha asilimia 90 ya mapato yote yatokanayo na shughuli za madini kubaki nchini kwa lengo la kuwanufaisha watanzania.
Kuhusu wachimbaji wadogo wa madini, Mavunde amesema kuwa, Serikali kupitia Sekta ya Madini imefanikiwa kununua mitambo 15 ya uchorongaji miamba, kutoa leseni 511 kwa vikundi vya wachimbaji wadogo katika mikoa ya Geita na Shinyanga pamoja na kuwapatia mkopo wa shilingi bilioni 30 kupitia taasisi za fedha kama njia mojawapo ya kuwezesha kuendelea na shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini.
Ameongeza kuwa Serikali imefanikiwa kuweka mpango wa kununua mitambo mikubwa aina ya CIP yenye uwezo wa kuchenjua tani 120 kwa saa pamoja na kuanzisha mfuko wa dhamana ili kuwawezesha na kuwajengea uwezo wachimbaji.

Amesema Katika kuhakikisha utoaji wa taarifa sahihi za kiuchunguzi wa maabara kwa sampuli za madini na miamba,serikali kupitia taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imefanikiwa kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika mkoa wa Dodoma,Geita na Chunya kwa lengo la kuongeza wigo wa huduma ndani na nje ya nchi. Aidha Tanzania na Taasisi Jiolojia ya Finland (GTK) kwa pamoja zimekubaliana kuwajengea uwezo wa kitaalamu watumishi wa GST.

