Na Lucy Ngowi
KATIKA kuadhimisha miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeeleza kuwa sekta ya elimu imepitia mageuzi makubwa yaliyowezesha kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu na kuinua ubora wake.
Rais wa CWT, Dkt. Suleiman Ikomba, amesema hayo leo Disemba tisa, 2025, akibainisha kuwa tangu enzi za Elimu ya Kujitegemea hadi mabadiliko ya sasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hatua kubwa zimepigwa.
Amesema mara baada ya Uhuru, serikali ilijikita katika kupanua shule za msingi vijijini na kuongeza uandikishaji kupitia kampeni ya Elimu ya Msingi kwa Wote.
Amesema kipaumbele kwenye kusoma, kuandika na kuhesabu kuliweka msingi thabiti kwa mfumo wa elimu uliokuwa unakua.
Amesema kuanzia mwaka 1995 hadi 2010, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na ule wa Sekondari (MMES) uliwezesha ujenzi na upanuzi wa shule katika kila kata, kupunguza uwiano wa mwanafunzi kwa mwalimu na kuongeza ufaulu.
“Mwaka 2015, serikali ilizindua rasmi sera ya Elimu Bila Ada, hatua iliyoleta ongezeko kubwa la wanafunzi, ujenzi wa madarasa, maabara na mabweni, pamoja na maboresho ya mitaala inayolenga ujuzi na fikra pevu,” amesema.
Kwa mujibu wa Dkt. Ikomba, miaka ya 2020 hadi 2025 imeonyesha kasi mpya kupitia elimu ya kidijitali, kuimarika kwa TEHAMA shuleni na mkazo katika ujuzi wa karne ya 21 kama ubunifu, teknolojia na stadi za maisha.
Katika ujumla wa miaka 64 ya Uhuru, Tanzania imejikita katika kudumisha amani, mshikamano na diplomasia imara, huku elimu ikiendelea kuwa injini ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutoka falsafa ya Elimu ya Kujitegemea hadi mfumo unaoangazia ubunifu na teknolojia za kisasa.

