Na Lucy Lyatuu
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amezindua mita Janja (Smart Meters) za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), zinazotumia mfumo mpya wa kisasa na kuagiza zisambazwe nchi nzima na wateja wapya wafungiwe mita hizo.
Amesemamita hizi zina mfumo unaolenga kuboresha utoaji wa huduma za umeme nchini na kuongeza ufanisi kwa Shirika na wateja wake.
Akizungumza katika hafla hiyo Ndejembi ametoa pongezi kwa TANESCO kwa hatua kubwa ya kimapinduzi waliyoifikia katika maboresho ya huduma kwa umma.
Ameiagiza Tanesco kuanzisha mfumo utakaorahisha muingiliano kati ya Shirika na wateja wake ikiwa ni mwendelezo wa kuendana na kasi na mapinduzi ya teknolojia ya sasa.

Kadhalika ameishauri Tanesco kuendelea kuboresha mawasiliano ya mara kwa mara na wateja ili kuimarisha utoaji huduma wa kisasa.
“Uzinduzi wa Mita Janja hizi ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia , kuhakikisha wananchi wanapata umeme bora, wa uhakika na unaoendana na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa,” amesema.
Waziri Ndejembi amekumbusha changamoto ambazo wateja walikuwa wanakutana nazo kwa kutumia mita za zamani, ikiwemo kushindwa kuona matumizi ya umeme kwa wakati halisi, ugumu wa kupanga bajeti, pamoja na hitilafu mbalimbali kama tokeni kushindwa kuingia, kupotea kwa kumbukumbu au kuharibika kwa rimoti za kuingiza tokeni.

Ameeleza kuwa baadhi ya mita zilikwekwa katika maeneo magumu kufikika, hali iliyowalazimu wateja kupanda ngazi au stuli kila wanaponunua umeme, jambo lililosababisha usumbufu mkubwa hasa wakati wa dharura.
Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Mita Janja ni matokeo ya uamuzi wa Serikali na TANESCO kupambana na changamoto hizo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Amesema kupitia mita hizo mpya, wananchi wataweza, kuingiza umeme popote walipo bila kulazimika kufika nyumbani,kufuatilia matumizi yao kwa muda halisi kupitia mfumo mahiri na kupata taarifa za kuisha kwa umeme kwa wakati kupitia kiashiria (alert).
Amesema mita hizo zitasaidia kubaini wizi wa umeme, kutambua uharibifu wa mita, na kupunguza upotevu wa nishati kwa wakati halisi, hivyo kuimarisha mapato ya shirika na kulinda fedha za Serikali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange amesema mita hizo zinafaida ikiwemo kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu, zina suluhisho endapo mteja akinunua umeme kwa bahati mbaya.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema sekta ya nishati inakuwa kwa teknolojia kwa kiwango kikubwa.


