Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Palamagamba Kabudi, amepongeza kampuni ya E & D Vision Publishing baada ya kutembelea banda lao katika Maonesho ya 32 ya Kitaifa ya Vitabu Tanzania yanayoendelea katika viwanja vya Maktaba Kuu, Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya Waziri Kabudi kutembelea banda hilo, Meneja wa E & D Vision Publishing, Tumsifu Usiri, amesema maarifa ni nguzo muhimu katika kumjenga mtu anayejiamini na anayejitambua.

Meneja huyo ameyasema hayo Novemba 21, 2025, wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo ambayo yamefunguliwa rasmi na Waziri Kabudi.
Amesema kampuni hiyo ipo makini kuhakikisha vitabu wanavyozalisha vinawafikia Watanzania wa makundi yote.
Amesema ushiriki wao katika maonesho hayo ni fursa muhimu ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya vitabu nchini.
Amefafanua kuwa E & D Vision Publishing inachapisha vitabu kuanzia ngazi ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.
Pia huchapisha vitabu vya maarifa mbalimbali, ikiwemo kitabu kinachohusu Mlima Kilimanjaro pamoja na vitabu vya watu mashuhuri serikalini wakiwemo Juma Mwapachu, Barnaba Samatta, Richard Mabala na wengineo.
Aidha, kampuni hiyo inachapisha vitabu vya nukta nundu (Braille) kwa ajili ya watu wenye uoni hafifu na wasioona kabisa, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha kila mtu anafikiwa na huduma ya maarifa bila vikwazo.
Amesisitiza, “Maarifa yatokanayo na usomaji wa vitabu ni chakula cha nafsi. Vitabu ni tiba muhimu ya afya ya akili. Maarifa yanaunda jamii yenye nidhamu na mwanga wa fikra.”


