Na Lucy Lyatuu
MADIWANI na Wenyeviti wa serikali za mitaa ya Ilala, Temeke na Kigamboni, Dar es Salaam wamehimizwa kuwasaidia wananchi kufahamu hatua sahihi za kutoa taarifa za hitilafu za umeme kupitia mfumo mpya wa Nihudumie, ambao unatoa huduma kwa haraka na bila gharama.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ametoa rai hiyo Dar es Salaam wakati akifungua kikao kazi kilichoandaliwa na (TANESCO) kwa ajili ya kuwakutanisha viongozi hao.
Amewataka viongozi hao kushirikiana kikamilifu na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili kuwezesha utoaji wa huduma bora na ya uhakika ya umeme kwa wananchi.
Amesema sifa ya kiongozi bora ni kuishi na kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo hitaji la umeme wa uhakika na kuwasihi kuendelea kushirikiana na Tanesco ili kuhakikisha changamoto za upatikanaji wa umeme zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema serikali inatambua na kuthamini ushirikiano unaoendelea kati ya viongozi wa serikali za mitaa na TANESCO, katika kuhakikisha huduma za umeme zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
Kuhusu huduma ya umeme, amesema viongozi wa serikali za mitaa wana nafasi ya kipekee katika kusimamia masuala ya umeme kwa kuwa wao ndio wapo karibu na wananchi.
Mpogolo amesisitiza umuhimu wa viongozi kusimamia ulinzi wa miundombinu ya umeme, ikiwemo nguzo na nyaya, hasa katika maeneo ya mijini ambayo yanakabiliwa na uharibifu kutokana na shughuli za ujenzi ambapo baadhi ya uharibifu huo husababishwa na watu wanaounganisha umeme kiholela, jambo linalosababisha madhara kwa jamii.
Amewataka viongozi wa wilaya na TANESCO kuendeleza mafunzo kama hayo katika maeneo mengine ya jiji ili kuongeza uelewa na kuboresha mahusiano baina ya viongozi na shirika hilo huku akiwashukuru waliojitokeza licha ya majukumu yao mengi.
“Kutenga muda wa kushiriki mafunzo haya ni ishara ya kujitoa katika kuhudumia wananchi, jambo ambalo limewezesha TANESCO kutekeleza dhamira yake ya kutoa elimu na kupokea changamoto zinazowakabili wananchi kwenye maeneo yao,’amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Irene Gowele, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO LazaroTwange, amesema TANESCO imeanzisha mkakati wa kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mitaa ili kuboresha upatikanaji wa taarifa, kuharakisha huduma na kutatua changamoto za umeme kwa ufanisi zaidi.
Amesema kupitia mafunzo na majadiliano yao, viongozi hao wataelezwa miradi ya kimkakati inayoendelea katika maeneo yao na namna wanavyoweza kuwa daraja la mawasiliano kati ya wananchi na shirika.
Aidha, amebainisha kuwa serikali kwa sasa inaelekeza nguvu katika kuwahudumia wananchi moja kwa moja, na hivyo ushirikiano na viongozi wa mitaa ni muhimu.

