Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema anaamini katika uongozi wa kimfumo unaoheshimu mipangilio ya kiutawala, badala ya kutegemea sifa za mtu mmoja.
Aidha amesema mambo mazuri yanayofanywa katika Wizara yanapaswa kuwa ya pamoja ili kuongeza ufanisi na tija.

Simbachawene ameyasema hayo wakati akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Innocent Bashungwa, katika hafla iliyofanyika Mtumba jijini Dodoma.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi na watumishi wa Wizara kushirikiana, kukumbushana na kusaidiana ili kuhakikisha majukumu yote yanatekelezwa kwa ufanisi
Pia ameahidi kuendeleza misingi na miradi mizuri iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Bashungwa, ikiwemo kuendeleza rasilimali zilizokuwa zimeanza kutumika kwa ajili ya kuisukuma Wizara hiyo kwenda mbele.

Kwa upande wake, Bashungwa ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wowote atakapohitajika.

