Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Mufindi Kaskazini, Exaud Kigae, amemtaja Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba kuwa ni miongoni mwa mawaziri mahiri nchini.
Aidha Nchemba ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa katika chama, serikalini, na hata katika jamii kwa ujumla.
Amesema hayo leo Novemba 13, 2025 katika viwanja vya Bunge baada jina la Nchemba kuthibitishwa na wabunge.
Kigae amesema moja ya dalili za umahiri wa Waziri Mkuu huyo ni namna alivyohakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi tangu alipokuwa Waziri wa Fedha.
Ameongeza kuwa, kupitia usimamizi wake, mapato ya serikali yameongezeka na utekelezaji wa bajeti umeleta matokeo makubwa yaliyowezesha taifa kuona mafanikio ya kiuchumi.
“Kwa uwezo wake huo, tunaamini ataendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na miradi mbalimbali ya kimkakati.
“Hasa katika kipindi hiki ambapo serikali inalenga kuboresha miundombinu wezeshi na kukuza uchumi katika sekta mbalimbali,” amesema Kigae.
Aidha, amebainisha kuwa kuthibitishwa kwa jina la Dk. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu ni hatua sahihi, kwani ni miongoni mwa viongozi wanaoweza kusimamia dira ya taifa ya Tanzania ya 2050 na kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya CCM unafanyika ipasavyo.

