Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Liwale mkoani Lindi, Mshamu Munde, ameapishwa rasmi leo, Novemba 12, 2025, na kuahidi kushirikiana na wananchi kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.
Ahadi hiyo ameitoa muda mfupi baada ya kuapishwa katika viwanja vya Bunge alipozungumza na waandishi wa habari.
Munde amesema anaingia bungeni akiwa na dhamira ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Liwale, hususan tatizo la miundombinu ya barabara, kilimo na huduma za kijamii.
“Changamoto kubwa kwa muda mrefu imekuwa ni barabara ya Liwale–Nangurukuru, ambayo inaunganisha barabara kuu ya Lindi–Dar es Salaam. Tatizo hili sasa linapatiwa ufumbuzi kupitia Ilani ya CCM,” amesema.

Kwa mujibu wa Ilani hiyo, barabara ya Liwale–Nangurukuru itajengwa kwa kiwango cha changarawe chenye madaraja na mitaro bora, ili iweze kupitika kwa mwaka mzima.
“Barabara hii ikikamilika itakuwa mkombozi wa kiuchumi. Wananchi hawatalazimika tena kupanga safari kutokana na mvua, na usafirishaji wa mazao utaimarika,” amesema Munde.
Aidha, amesema barabara ya Liwale–Nachingwea itajengwa kwa kiwango cha lami, hatua itakayowezesha wananchi kupata mtandao mzuri wa usafiri kuelekea Lindi na Dar es Salaam, hivyo kuchochea biashara na uwekezaji.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Munde amesema wakati huu Liwale inategemea zaidi zao la korosho, lakini amepanga kuhamasisha uzalishaji wa ufuta, alizeti na chikichi ili kuongeza vyanzo vya mapato.
“Tukifanikiwa kuwa na mazao manne ya uhakika, kipato cha wananchi kitaongezeka mara nne kwa mwaka,” amesema.
Mbunge huyo amehitimisha kwa kusema ataendelea kushirikiana na serikali kuboresha huduma za elimu, afya na maji, akisisitiza kwamba maendeleo ya Liwale yatachochewa zaidi kwa ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na viongozi wao.

