Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Exaud Kagae, amesema ana matumaini makubwa kuwa, Waziri Mkuu ajaye atakuwa kiongozi thabiti, mwenye dira na uwezo wa kusimamia ajenda kuu za maendeleo ya taifa.
Kagae amesema hayo leo Novemba 12, 2025 katika viwanja vya Bunge alipozungumza na Waandishi wa Habari, ambapo kesho Novemba 13, 2025 bunge linaenda kuthibitisha jina la Waziri Mkuu ajaye.

Amesema uteuzi wa Waziri Mkuu ajaye ni hatua muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo ya Taifa ya 2020 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo ndiyo msingi wa serikali inayoundwa.
“Tunatarajia kupata Waziri Mkuu atakayesimamia ajenda za kitaifa kwa ufanisi, atakayehakikisha maendeleo endelevu yanafikiwa na kumsaidia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza kasi kubwa ya maendeleo tuliyoiona katika miaka minne iliyopita,” amesema Kagae.
Akimpongeza Rais Samia kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi chake cha uongozi, Kagae amesema maendeleo hayo yameleta mabadiliko makubwa hata katika jimbo lake la Mufindi Kaskazini.
“Ninakiri wazi kwamba mafanikio ya serikali ya awamu ya sita yamenisaidia sana katika jimbo langu. Tumetekeleza miradi mikubwa ya kihistoria, kuanzia ujenzi wa barabara za lami vijijini, upatikanaji wa maji safi, kuboreshwa kwa huduma za afya na elimu, hadi miradi ya miundombinu inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja,” amesema.
Mbunge huyo amesema ana imani kuwa Waziri Mkuu ajaye ataendeleza kasi hiyo ya maendeleo, kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati, na kuleta tija kubwa zaidi kwa wananchi.
“Tunataka kiongozi ambaye atakuwa bega kwa bega na Rais Samia kuhakikisha maendeleo yaliyopatikana katika miaka minne iliyopita yanaongezeka mara mbili zaidi. Hii itawezekana tu kwa Waziri Mkuu jasiri na mwenye ufuatiliaji makini wa kazi za serikali,” amesema.
Kagae pia aliwashukuru wananchi wa Mufindi Kaskazini kwa ushirikiano waliomuonyesha katika kipindi kilichopita na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kwa ukaribu katika muhula huu wa pili.
“Ninawashukuru wananchi wangu kwa kuniunga mkono kwa dhati. Tumeanzisha miradi mikubwa ambayo haijawahi kufanyika, na naamini katika kipindi cha 2025 hadi 2030 tutazidi kufanikisha zaidi. Wakati huu tutazidi kuandika historia ya maendeleo katika jimbo letu,” amesema.

