Na Mwandishi Wetu
MOROGOEO: MGOMBEA urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema njaa na tatizo la ajira vitaendelea kuiumiza nchi endapo wananchi hawataachana na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na wananchi wa Morogoro Mjini Oktoba 20, 2025, Mwalim amewataka Watanzania wasicheke na CCM bali wachukue maamuzi sahihi ili wanufaike na rasilimali zao.
“Uchumi wa nchi unaangalia cooperative advantage ili kukua kiuchumi kama ilivyo China. Kwanini? Kwa sababu uzalishaji wao ni rahisi kwa kutumia teknolojia,” amesema.
Ameongeza kuwa China ndiyo inayotengeneza bidhaa za nchi kama Marekani, Ujerumani na Tanzania, kutokana na kuwekeza kwenye teknolojia.

Mwalim amesema Tanzania imejaliwa kila kitu madini, ardhi yenye rutuba na maji ya kutosha lakini bado wananchi wake wanaishi katika umasikini.
“Leo madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania, lakini ukienda Ulaya unaambiwa yanatoka Kenya… hizi ndiyo akili za CCM,” amesema.
Amedai kuwa Watanzania wanaendelea kukosa ajira huku Wakenya wakinufaika na kilimo na mazao yanayotoka Tanzania.
Aidha, amejigamba kuwa hakuna mgombea mwingine aliyesafiri kilometa nyingi zaidi yake katika kipindi cha kampeni, akibainisha kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilimkabidhi gari lililotembea kilometa 500, lakini hadi sasa limefika zaidi ya kilometa 10,000.

