Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ameshuhudia tukio la Benki ya CRDB ikisaini ubia mkubwa wa kimkakati na taasisi tatu za fedha za kimataifa wenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 300, kwa ajili ya kuendeleza ujumuishwaji wa fedha na maendeleo endelevu barani Afrika, tukio lililofanyika jijini Washington D.C., nchini Marekani.
Benki ya CRDB imeingia katika ushirikiano huo na FinDev Canada, DEG (KfW Group, Ujerumani), na Shelter Afrique Development Bank (ShafDB), ikiwa ni hatua muhimu katika safari ya benki hiyo ya kuendeleza ujumuishwaji wa fedha na maendeleo endelevu barani Afrika.

Hati za Makubaliano (MoUs) zilisainiwa wakati wa Jukwaa la Wabia na Wawekezaji “Investors and Partners Forum” lililofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na IMF jijini Washington D.C.
Jukwaa hilo la kimataifa lililoandaliwa na Benki ya CRDB lilikutanisha wawekezaji wa kimataifa na viongozi wakuu wa serikali kutoka Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Viongozi mbalimbali wa kimataifa walishiriki jukwaa hilo ikiwemo Waziri wa Fedha wa Burundi, Waziri wa Habari wa DRC, Magavana wa Benki Kuu za Tanzania na Burundi, Mabalozi wa Tanzania na Burundi nchini Marekani, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Tanzania, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mikutano ya Benki ya Dunia na IMF na ambae pia alikuwa Mgeni Rasmi katika jukwaa hilo.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, pamoja na viongozi wakuu wa taasisi washirika: Mkurugenzi Mtendaji wa Shelter Afrique Development Bank Thierno-Habib Hann, Mkurugenzi Mtendaji wa DEG Roland Siller, na Mkurugenzi Mtendaji wa FinDev Canada Lori Kerr.

Ukuaji Jumuishi: Kupitia ushirikiano na FinDev Canada, Benki ya CRDB imepata uwezeshwaji wa Dola za Kimarekeni Milioni 60 zinazolenga kupanua mikopo kwa wajasiriamali wachanga, wadogo, na wa kati (MSMEs), kukiwa na msisitizo maalum kwenye biashara zinazoendeshwa na wanawake na miradi inayohimili mabadiliko ya tabianchi.
Uwezeshaji wa Biashara Ndogo na za Kati (SME): Kupitia DEG, Benki ya CRDB itatoa Dola za Kimarekani Milioni 50 kwa ajili ya mikopo midogo midogo ya biashara ndogo na za kati (SME), kusaidia ukuaji wa biashara, ubunifu, na uzalishwaji wa ajira nchini Tanzania.
Kuhusu Usawa wa Kijamii na Makazi Nafuu, Ushirikiano na Shelter Afrique Development Bank unalenga kupunguza upungufu wa makazi katika kanda, ambapo kwa kuanzia Benki ya CRDB imepokea Dola za Kimarekani Milioni 10 kwa ajili ya kampuni tanzu yake ya nchini DRC.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, DKT. Natu El-maamry Mwamba, ametoa wito kwa jumuiya ya Kimataifa kwewekeza mitaji na teknolojia nchi Tanzania kutokana na fursa mbalimbali zilizomo ikiwemo soko la uhakika la biashara, sera nzuri na vivutio mbalimbali vya uwekezaji.