Na Lucy Ngowi
MBEYA: MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango amewasihi Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa kulinda amani, uhuru na mshikamano wa taifa ili kuepuka kupoteza tunu hizo muhimu.
Akizungumza katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yaliyofanyika mkoani Mbeya, Dkt. Mpango amesema jamii inapaswa kukemea mmomonyoko wa maadili, rushwa na ufisadi.

“Vitendo vya mmomonyoko wa maadili na rushwa ni miongoni mwa mambo yanayohatarisha tunu tulizoachiwa na waasisi wetu kama Hayati Mwalimu Nyerere,” amesema Dkt. Mpango.
Aidha, amewasihi wananchi kuhifadhi mazingira kwa kulinda vyanzo vya maji na kupanda miti, akisisitiza kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa kuigwa katika maeneo hayo.

Akizungumzia Mwenge wa Uhuru, Dkt. Mpango amesema ulipoanzishwa ulilenga kuonyesha madhara ya udhalimu wa mkoloni na kuhamasisha amani. “Serikali itaendelea kuenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru katika taifa letu,”.
Kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Vijana, amesema asilimia 77.3 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 35, hivyo ni muhimu kwa serikali kutambua mchango wa kundi hilo.
Aliwahimiza vijana kutumia nguvu zao katika ubunifu na maarifa, huku akieleza kuwa Serikali inawaunga mkono. Pia amewataka Wizara ya Elimu Tanzania Bara na Visiwani kutumia kitabu cha Mwenge wa Uhuru alichokizindua kama nyenzo ya kufundishia ili kuendeleza uelewa kwa vijana.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amesema vijana 142,000 kutoka nchi nzima wameshiriki katika midahalo na makongamano yaliyolenga kuwaelimisha.

Alieleza kuwa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 umefanyika mkoani Pwani, huku ule wa 2026 ukitarajiwa kufanyika Kusini Pemba na kilele chake kufanyika Rukwa.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ismail Ally Ussi kutoka Kaskazini Unguja, amesema waliukabidhi Mwenge huo kwa Dkt. Mpango Aprili 2, 2025 mkoani Pwani. Alibainisha kuwa miradi ya maendeleo 1,382 yenye thamani ya Sh Trilioni 2.87 ilikaguliwa, na yote ilikubaliwa.
Katika misa takatifu ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Asizi, Mwanjelwa – Mbeya, Dkt. Mpango aliwaomba Watanzania kuendelea kumuombea Baba wa Taifa ili aendelee kupumzika kwa amani na awe mmoja wa Watakatifu.
Amesema ni muhimu kila mmoja, hususan viongozi, kufuata mfano wa uaminifu wa Baba wa Taifa ambaye alilitakia mema taifa wakati wote.
Kwa niaba ya Serikali, Dkt. Mpango amewashukuru waumini na wananchi wa Mbeya kwa kujitokeza kumuombea Mwalimu Nyerere wakati wa kumbukizi ya miaka 26 tangu kifo chake.
Ibada hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga, aliyesema Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa maadili, haki, huruma, unyenyekevu na uaminifu.
Askofu Nyaisonga alisema Mwalimu aliacha urithi wa kisiasa, muungano wa taifa, mageuzi ya kidemokrasia na Azimio la Arusha la mwaka 1967 lililolenga usawa wa kijamii na kiuchumi. Aidha, alisisitiza kuwa Nyerere alitanguliza elimu, maadili, utamaduni wa Kiswahili, utu na maslahi ya taifa.