Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe amekagua huduma zinazotolewa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania ( TVLA), katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Uvuvi Jijini Dodoma na kuridhika nazo.
Profesa Shemdoe amekagua huduma hizo alipotembelea taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kujiridhisha na huduma zitakazotolewa kwa Wafugaji, Wavuvi na wadau mbalimbali watakaotembelea Maonesho hayo.
Huduma zilizokaguliwa na Katibu Mkuu huyo kwenye banda la TVLA ni pamoja na elimu ya uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama, elimu ya matumizi sahihi ya Chanjo za Mifugo na elimu ya uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo,.
Pia elimu ya usajili na uhakiki wa ubora wa viuatilifu vya Mifugo, elimu ya utafiti wa magonjwa ya wanyama pamoja na elimu kuhusiana na mafunzo kwa wataalamu wa Mifugo inayotolewa na TVLA.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania inashiriki Maonesho ya Nanenane kwa lengo la kutoa elimu ya huduma bora za maabara za Veterinari, kutoa elimu ya utafiti juu ya magonjwa ya wanyama na wadudu waenezao magonjwa hayo ndani na nje ya Tanzania.