Na Lucy Ngowi
GEITA: KATIBU Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Zena Ahmed Said, ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa juhudi zao za kuwafikia wananchi kupitia huduma za kimtandao, ikiwemo wale wasio na simu janja.
Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Geita, Zena amesema bado kuna idadi kubwa ya Watanzania wasiofahamu umuhimu wa kuwekeza katika mifuko ya serikali, hivyo ni jukumu la NSSF kuendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha kuhusu fursa hizo.

“Watakapowekeza katika mifuko yenu, mtawapa pia elimu ya uwekezaji. Nimefurahishwa na namna mnavyowafikia hata wale wasio na simu janja, maana bado wengi hawana vifaa hivyo. Kukosekana kwa njia mbadala ya kuwafikia kunawafanya waonekane kama wametengwa, lakini ninyi mmeamua kuwafuata popote walipo,” amesema Zena.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NSSF,Lulu Mengele, , amesema mfuko huo unatoa huduma kwa wananchi walioko kwenye sekta binafsi pamoja na wale walioajiriwa, wakiwemo wafanyakazi wa sekta ya madini.
Ameongeza kuwa katika banda lao mkoani Geita, NSSF inatoa huduma mbalimbali na kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mengele amebainisha pia kuwa kutokana na mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika mwaka 2018, NSSF kwa sasa haina ushindani wa moja kwa moja katika sekta ya hifadhi ya jamii, kwani wafanyakazi wote wa upande wa Tanzania Bara wanachangia NSSF, huku upande wa Zanzibar wakiwa chini ya ZSSF.
Akizungumzia utendaji wa mfuko huo, amesema kuwa thamani ya NSSF iliongezeka kutoka Sh. trilioni 4.8 wakati Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani, hadi kufikia trilioni 9.9 kufikia mwezi Juni, 2025.