Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WIZARA ya Kilimo imeshiriki kwa mafanikio makubwa katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa na teknolojia mbalimbali za kilimo,
Aidha kuwajulisha wananchi juhudi za serikali katika kuhakikisha usalama wa chakula na lishe kwa Watanzania wote.
Akizungumza katika maonesho hayo, Ofisa Kilimo Mkuu wa Wizara hiyo, Magreth Natai, amesema lengo kuu la ushiriki wao ni kutoa elimu kwa watanzania kuhusu wizara na taasisi zake zinavyohakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula.
“Tumejipanga vyema kuhakikisha tunafikia malengo ya usalama wa chakula na lishe kwa kuwa na dira na mikakati mbalimbali kama vile kuongeza tija katika uzalishaji, kudhibiti upotevu wa mazao kupitia kilimo cha umwagiliaji na ujenzi wa maghala ya kisasa,” amesema.
Amesema Wizara imeweka mkazo mkubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya kilimo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maghala katika ngazi ya halmashauri na kaya.
Amesema hatua hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza upotevu wa mazao ya chakula kutoka asilimia 30-40 hadi chini ya asilimia 20, huku lengo likiwa ni kufikia asilimia tano.
Katika banda la wizara hiyo, wananchi wamekuwa wakipata elimu juu ya matumizi ya mbegu bora, matumizi ya zana za kisasa za kilimo, mifumo ya taarifa za bidhaa, pamoja na mbinu bora za kuhifadhi chakula ili kukabiliana na sumukuvu na upotevu wakati wa mavuno.
“Tumekuwa na mafanikio makubwa. Kwa zaidi ya miaka 10 sasa, nchi yetu imekuwa ikijitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 100.
“Mwaka huu pekee tunakadiria kuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 128,” amesema.
Amewataka wananchi kufika kwenye mabanda ya wizara na taasisi zake ili kujifunza kwa kina kuhusu fursa zilizopo katika kilimo, pamoja na kupata majibu ya maswali kuhusu mbegu bora, pembejeo na teknolojia mpya zinazosaidia wakulima kuongeza tija na kipato.
Ametaja Taasisi na bodi zilizopo chini ya wizara ya kilimo ni Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Tanzania (TOSCI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA),
Pia Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Tengeru (MATI Tengeru), Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Ukiriguru (MATI Ukiriguru), Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Igurusi (MATI Igurusi),
Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Ilonga (MATI Ilonga), Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Mtwara (MATI Mtwara), na
Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Nyegezi (MATI Nyegezi).
Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Bodi ya Sukari Tanzania , Bodi ya Kahawa Tanzania, Bodi ya Chai Tanzania, Bodi ya Korosho Tanzania na Bodi ya Pamba Tanzania.
Vile vile Bodi ya Tumbaku Tanzania, Bodi ya Mazao ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Bodi ya Pareto Tanzania.